Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yajipanga kuwajibu wanaoiingilia Tanzania

27564 Ccm+pic TanzaniaWeb

Sat, 17 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinajiandaa kutoa msimamo wake kutokana na mvutano wa kidiplomasia unaoendelea kati ya Tanzania na baadhi ya mataifa ya Ulaya ukiwamo waraka uliotolewa na Umoja wa Ulaya (EU) ukilaumu kuzorota kwa hali ya kisiasa nchini.

Katika wiki za hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matamko kutoka katika baadhi ya mataifa ya nje zikilalamikia masuala ya kisiasa na haki za binadamu.

Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, kanali mstaafu Ngemela Lubinga akizungumza na Mwananchi jana alisema chama hicho kitaweka msimamo wake kutokana na hali hiyo inayoendelea.

Alisema CCM imeanza kukusanya taarifa kuhusiana na yale yote yanayoendelea na itatoa taarifa baada ya kujiridhisha na kile inachokikusanya.

Alisema chama kimelazimika kufanya hivyo ili kuepusha mkanganyiko wa mambo ambao unaweza kujitokeza kutokana na matamko yanayoendelea kutolewa washirika wa maendeleo.

Wakati chama hicho tawala kikijipanga kuchukua hatua hiyo, Serikali ya Sweden jana ilidhibitisha kumwita balozi wa Tanzania nchini humo, Dk Willbrod Slaa ikisema ilifanya hivyo ili kujadiliana naye kuhusiana na hali inavyoendelea nchini.

Ofisa wa ubalozi wa Sweden nchini, Ludvig Bontell aliliambia Mwananchi kuwa Dk Slaa aliitwa na wizara ya mambo ya nje nchini humo, juzi.

Alipoulizwa Dk Slaa alichoelezwa, Bontell alisema ujumbe aliopewa ni kama ule uliotolewa na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini.

Katika ujumbe wake, Mogherini alisema nchi wanachama wa EU zinatiwa wasiwasi na hali ya kisiasa inayoendelea nchini ikiwamo kuzuiwa kwa uhuru wa vyombo vya habari na kubinywa kwa vyama vya siasa.

Juhudi za Mwananchi kutaka kupata maoni kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahige au Msemaji Mkuu wa Serikali hazikuzaa matunda kwani mara zote simu zao ziliita bila kupokewa.

Akizungumza baada ya kuombwa kutoa maoni yake kuhusu sakata hilo, Profesa Kitojo Wetengere wa Chuo cha Diplomasia (CFR) alisema nchi hizo zinafanya hivyo kwa vile zinatambua Tanzania ni nchi maskini ikiendelea kutegemea misaada kutoka nje.

“Inabidi ifike wakati lazima tusimame imara dhidi ya nchi za Magharibi na tuendelee kujenga uhusiano na nchi za Afrika na mataifa mengine yaliyo rafiki ambayo yanaweza kutusaidia bila kuingilia mambo yetu,” alisema Profesa Wetengere.

Alihoji baadhi ya mataifa duniani yanajitazama kama polisi wa dunia, “Wanazungumzia uvunjifu wa haki za binadamu, walifanya nini wakati Marekani ilipoishambulia Libya? Hakuna chochote katika tamko la EU zaidi kuleta ukoloni mambo leo.”



Chanzo: mwananchi.co.tz