Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yafikisha kata 40 bila kupingwa

9485 Pic+ccm TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefikisha kata 40 ambazo kimepita bila kupingwa baada ya washindani wao 10 zaidi kutoka vyama vya upinzani kujitoa wakati kampeni zikiendelea.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imethibitisha kuwa hadi sasa CCM imeshajikusanyia madiwani 40 katika kata 77 zinazoshiriki uchaguzi mdogo.

Mbali na kata hizo, uchaguzi huo mdogo utafanyika pia katika Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma, Agosti 12, 2018.

Akizungumza na MCL leo Jumanne Julai 31, 2018, mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Dk Athuman Kihamia amesema, “Hadi kufikia leo (Julai 31, 2018) wagombea udiwani katika kata 40 kati ya 77 wamepita bila kupingwa kufuatia kujitoa kila siku kwa wagombea wengine.”

“Idadi hiyo ni ongezeko la wagombea 10 waliojiengua ukilinganisha na wale 30 wa awali” alisema bila kutaja kata hizo.

Mapema kabla ya uteuzi, baadhi ya wagombea kutoka vyama vya upinzani walienguliwa kwa sababu mbalimbali na kusababisha CCM ipate kaya 30 ilizokuwa imepita bila kupingwa.

Kufuatia hatua hiyo, wagombea 25 walikata rufaa katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambapo wagombea 10 walishinda na kurejeshwa kuendelea na uchaguzi na 15 rufaa zao hazikufanikiwa.

Katika uchaguzi huo, vyama kumi na mmoja vimesimamisha wagombea katika kata mbalimbali ambavyo ni ACT-Wazalendo (wagombea 17), ADC (3), CCM (77), Chadema (54), Chaumma (wawili), CUF (17), Demokrasia Makini (4), NCCR Mageuzi (6), NRA (3), SAU (1) na UPDP (2).

Katika Jimbo la Buyungu vyama vilivyosimamisha ni AAFP, ACT-Wazalendo, CCM, Chadema, CUF, DP, Demokrasia Makini, NRA, UMD na UPDP.

Chanzo: mwananchi.co.tz