Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yafichua siri ya ushindi uchaguzi mdogo

Ccmpicmm CCM yafichua siri ya ushindi uchaguzi mdogo

Tue, 20 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefichua siri tano za kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi mdogo uliofanyika juzi Desemba 17, 2022 katika jimbo la Amani visiwani Zanzibar pamoja na kata mbalimbali nchini.

Miongoni mwa sababu zilizobainishwa na chama hicho ni pamoja na uteuzi wa wagombea bora wanaokubalika katika maeneo husika na chama hicho kuaminiwa na wananchi na kupigiwa kura nyingi.

Siri zingine ni umoja na mshikamano uliopo ndani ya chama, kampeni za kisasa zilizowafikia wapigakura, uadilifu na uaminifu katika kuwatumikia wananchi hususan katika kukidhi matarajio yao katika kuwaletea maendeleo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Desemba 19, 2022 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Shaka Hamdu Shaka, chama hicho kimeshinda bila kupingwa katika kata tano kati ya 12 zilizofanya uchaguzi.

Shaka anazitaja kata hizo kuwa ni Dabalo (Dodoma), Ibanda (Mbeya), Misugusugu (Pwani), Kalumbeleza (Rukwa) na Lukozi (Tanga).

“Kazi ambayo inafanywa kwa weledi na ustadi mkubwa na serikali zake zikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Husein Ali Mwinyi kupitia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 ni wazi inawagusa wengi,” amesema Shaka.

Katika uchaguzi huo, CCM ilishindana na vyama vya upinzani katika kata za Majohe (Dar es Salaam), Mwamalili (Shinyanga) Njombe (Njombe), Vibaoni, Mnyanjani (Tanga), Mndubwe (Mtwara) na Dunda (Pwani).

Shaka kupitia taarifa hiyo amefafanua kuwa kushindwa kwa vyama vya upinzani ni mwendelezo wa ushahidi kwamba havikubaliki na Watanzania kwani wameendelea kuwathibitishia kwamba hawajazoea siasa za vurugu, ulaghai, ubinafsi na migawanyiko ambayo haina tija katika ustawi wa maisha na maendeleo yao.

Shaka aliahidi kwamba chama hicho litaendelea kuwatumikia Watanzania kwa amani na utulivu kwa kuwa kina uzoefu wa kufanya siasa za kistaarabu na maendeleo kwa ustawi wa Watanzania wote.

Chanzo: Mwananchi