Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yachuja majina wabunge EAC

SHAKA WEB CCM yachuja majina wabunge EAC

Mon, 5 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sekretariati ya Halmashauri Kuu ya CCM imekutana jana kuanza kuchuja majina ya makada 162 kutoka Tanzania Bara waliojitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama kuwania nafasi ya uwakilishi wa nchi katika Bunge la Afrika Mashariki (EAC).

Pia kwa wagombea 16 waliojitokeza kuwania uwakilishi kwa Zanzibar nao walianza kuhojiwa jana na Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM visiwani humo.

Sekretariati ya Halmashauri iliketi Jijini Dodoma jana katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete chini ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo kuhoji wagombea wa nafasi hiyo mmoja baada ya mwingine.

Katibu Mkuu wa NEC itikadi na Uenezi, Shaka Hamud Shaka katika taarifa yake ya kuwaita makada hao kufika Dodoma na Zanzibar kwenye usaili aliwataka wafike wakiwa na nyaraka zote zinazohusika.

Kazi hiyo ya kuhoji makada wanaoomba kuteuliwa inahusisha makada 178 waliojitokeza kuomba kuteuliwa, 162 wanahojiwa Dodoma na 16 Zanzibar.

Mahojiano hayo yanafanyika Dodoma kwa siku mbili kuanzia jana Septemba 4 hadi leo ili kupata watu 27 kutoka Tanzania Bara na sita kutoka Kamati Maalumu Zanzibar ili kukamilisha orodha ya wagombea 33 watakaoteuliwa na chama ili majina yao yapelekwe katika vikao vya juu.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977, wagombea watakaoteuliwa na chama, majina yao yatapelekwa mbele ya Kamati ya Maadili ambayo inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana ili kuangalia maadili ya wagombea hao.

Yanayotazamwa yamefafanuliwa kwamba ni pamoja na uwajibikaji katika chama, tabia na mienendo pamoja na uadilifu wa mwanachama.

Makada watakaopenya katika hatua hiyo majina yao yatapelekwa mbele ya Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya CCM inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan ili kuthibitishwa kabla ya majina hayo kupelekwa Bungeni kupigiwa kura.

Bunge kwa mamlaka yake, litawapa fursa ya kujitambulisha na kujieleza wataifanyia nini Tanzania katika Bunge la EAC, kisha watapigiwa kura na Bunge zima ili kupata wabunge wawakilishi.

Taarifa rasmi ya majina yatakayoteuliwa na CCM itatolewa rasmi keshokutwa (Septemba 7, mwaka huu) na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM.

Mchakato wa kuwapata wagombea wanaoomba kuteuliwa na chama ulianza kwa kuchukua fomu Agosti mosi hadi Agosti 10, mwaka huu katika vituo vya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar.

HabariLeo jana iliweka kambi katika Viwanja vya Jakaya Kikwete na kushuhudia makada wakiwa wamevalia shati au bilauzi za kijani na suruali au sketi nyeusi kwa wanaume na wanawake kwa mfuatano wakiitwa kuhojiwa kwa kufuata alfabeti za majina yao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live