Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yaanika mafaili wanaojipitisha majimboni

Chongolo Awajibu Wanaosema Nchi Inakopa Sana.jpeg Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo.

Fri, 3 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama Cha Mapinduzi(CCM) kimefungua mafaili ya kukusanya taarifa za wanachama wanaokiuka maadili ikiwamo kujipitisha kwenye majimbo na kata kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Vilevile, kimetoa onyo kwa makatibu wa CCM kuanzia shina hadi mikoa watakaobainika kutowatenda haki wanachama na wanaoendekeza ulevi.

Akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida jana, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, alisema kwa sasa ni wakati wa kufanya kazi kwa kushikamana na kuacha chokochoko.

"Wakati wa kufanya kazi tushikamane, tuache chokochoko. Mbunge wa jimbo hili yupo na majimbo yote ya chama chetu sitegemei kumwona mtu anaanza kujipitisha, hapana! Vivyo hivyo kwa viti maalum, acheni watu wafanye kazi, subiri muda mwafaka.

"Sisi tumefungua mafaili, niwaambie si mmeona utaratibu wa mwaka jana kwenye chama mambo yalikuwaje, huyu kata, huyu kata, wanasoma sifa na matatizo yake, ninasema kata huyu, jamaa mlevi wa kupindukia, ninasema kata.

"Ushahidi upo? Ndio, ninasema kata, juzi amekutwa baa yupo hoi taabani wamembeba wamempeleka kwake. Hivi tunataka viongozi wa aina hiyo? Sasa kama kiongozi mwenye dhamana kubwa ndani ya chama kazi yangu nini? Kata, sitegemei kuona mtu anatembea kibunge au kidiwani kabla ya 2025, acheni watu wafanye kazi," alionya.

Alisema chama kimekamilisha kutengeneza safu ya uongozi kwa kipindi cha miaka mitano na uchaguzi umeisha, hivyo hategemei kuona nongwa.

"Katibu yeyote wa CCM kuanzia shina hadi mkoa tukisikia unakuwa wa kwanza kwenye viti virefu, hufai tukisikia una tabia ya kwenda kukopa kila nyumba, hufai kuwa kiongozi. Tukisikia hutendi haki, hufai kuwa kiongozi, tunataka kiongozi anayesimamia taratibu ambaye hafanyi mambo yanayokwenda kinyume cha taratibu," alisisitiza.

Akiwa wilayani Mkalama, Chongolo alisema sifa ya kiongozi wa CCM ni kuzungumzia matatizo ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi.

"CCM imepewa dhamana ya kuongoza nchi, hatuji kupiga porojo, sisi tunakuja kusikiliza wananchi na kuchukua changamoto zao na kuzitatua," alisema.

Chongolo alisema CCM haiwezi kufanya kazi ya kupiga kelele bali inahangaika na mambo ya wananchi.

"Kuna wengine wanakuja wanasema hakuna kilichofanyika, hebu angalieni tangu uhuru hadi sasa maendeleo yaliyofanyika kwenye sekta ya elimu, afya, miundombinu, kila nyanja imeguswa kwa maendeleo," alisema.

Chongolo yupo mkoani Singida na sekretarieti yake kwa ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM na kusikiliza kero za wananchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live