Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yaagiza wabunge waende majimboni

578549ed00d433ff458ff1387a8ae6e4.jpeg CCM yaagiza wabunge waende majimboni

Thu, 8 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewaagiza wabunge wa Bunge la Tanzania kupitia chama hicho wafanye ziara katika majimbo yao kueleza yaliyopitishwa na Bunge la bajeti na kupokea changamoto zingine.

Chongolo alitoa agizo hilo jana katika mji mdogo wa Laela Sumbawanga Vijijini kwenye kikao cha ndani cha viongozi wa CCM na serikali siku ya kwanza ya ziara ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya chama hicho mkoani Rukwa.

"Nawapongeza wabunge niliowakuta kwenye mikoa yao baada ya Bunge la bajeti, sasa kazi yenu wabunge ni kupita kwenye jimbo lote kuwaeleza wananchi yaliyopitishwa kwenye bajeti, yanayowagusa. Pia wabunge kaeni kwanza na madiwani muwasikilize ndipo mpange ratiba ya ziara zenu kwenda kwa wananchi."alisema.

Chongolo alisema wabunge kulalamika kuhusu bajeti ndogo ya Wakala wa Barabara Miji na Vijijini (Tarura) Rais Samia Suluhu Hassan alitoa shilingi milioni mia tano kwa kila jimbo kuimarisha barabara za vijijini na mijini.

"Natoa maagizo kwa wabunge wote nchini ambao ni zao la CCM kwa sasa wamemaliza bunge la bajeti, wabunge wote waende kwenye majimbo yao wakawaeleze wananchi yaliyomo kwenye bajeti na hususani yanayowagusa ili waelewe nini serikali inataka kufanya kwao"alisema.

Chongolo aliwataka viongozi wa CCM ngazi za mikoa, wilaya na kata waende kwenye mashina na matawi kufanya mikutano ya kuwasikiliza na kutoa muongozo wa CCM katika kutekeleza majukumu ya kila siku ili kubaini changamoto na kuzishughulikia kwa wakati.

Alisema wakati CCM inajiandaa kwa uchaguzi wa mwaka 2022, ni marufuku kupanga safu za uongozi.

Alisema wamemua kufanya ziara hiyo ili kila mkoa upate ujumbe kwa kutumia gharama ndogo kwani wakifika kwenye mkoa wanagawana wilaya na kila mjumbe wa sekretarieti ya CCM Taifa anaenda kwenye wilaya moja kufikisha ujumbe.

Aliagiza kamati za siasa za kata ziwapime madiwani katika kutimiza wajibu wao na za wilaya ziwapime wabunge na kamati ya siasa mkoa kufanya hivyo hivyo ili kuwa na taarifa sahihi za kila kiongozi wa CCM aliyeko kwenye nafasi za dola.

Chanzo: www.habarileo.co.tz