Dar es Salaam. Wakati vyama vya upinzani nchini Tanzania vikilalamika wagombea wake kuenguliwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, CCM wamesema wameondolewa kwa makosa ya kiufundi wakati wa kujaza fomu.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Novemba 7, 2019 jijini Dar es Salaam na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polpole wakati akieleza namna chama chake kilivyojipanga kunyakua ushindi kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019.
Polepole amesema CCM ilisambaza mawakili 1250 nchi nzima kwa ajili ya kukutana na wagombea wake na kuwafundisha namna ya kujaza fomu zao kabla ya kuziwasilisha kwa wasimamizi wa uchaguzi.
“Wapinzani mmeenguliwa kwa makosa ya kiufundi ambayo msingi wake ni ujinga, sisi (CCM) hatuhusiki,” amesema Polepole.
Amesema chama hicho tawala hakikuruhusu mgombea wake kujaza fomu wakiwa peke yao bila kuonana na mawakili waliopelekwa.
Amesema CCM ilianza maandalizi ya uchaguzi tangu mwaka 2017 na kwamba chama hicho kimewekeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa sababu ndiko oganaizesheni ya chama inakoanzia.
Mwanasiasa huyo amebainisha baadhi ya mambo ambayo yamewakosesha wapinzani kuteuliwa kuwa ni pamoja na kushindwa kujaza fomu kwa usahihi kwa kujaza kile ambacho kinatakiwa kwenye fomu hiyo.
“Moja ya sifa za mgombea ni awe na shughuli halali ya kumwezesha kuishi, sasa wenzetu wamekuwa wakiulizwa na wasimamizi wa uchaguzi ‘unafanya kazi gani?’ anajibu ‘tunapambana tu’. Sisi tumechagua watu wenye shughuli za kufanya, hata ukimuuliza atakwambia ‘mimi ni mkulima, nina heka zangu mbili nalima’,” amesema Polepole.
Amesema wengine wamekosea kugombea katika mitaa au vitongoji ambavyo hawaishi kwa sababu hawajui mipaka ya maeneo yao, kujikuta wakienguliwa kwa kuwa sio wakazi wa eneo husika.
Polepole amesema wanachama wengi wamejitokeza kutaka kugombea kupitia CCM ambapo idadi yao imefikia 930,717 nchi nzima.
Hata hivyo, amesema CCM imesimamisha wagombea 332,539 nchi nzima katika nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.