Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM wazoa kata tano Manyara

11663 Pic+manyara TanzaniaWeb

Mon, 13 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Babati.  Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Manyara kimeshinda kata tano ambazo awali zilikuwa chini ya Chadema na ACT-Wazalendo katika uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika jana Jumapili Agosti 12, 2018.

Akitangaza matokeo kata ya Bagara jana usiku mkurugenzi wa mji wa Babati,  Fortunatus Fwema amesema mgombea wa CCM, Nicodemus Tlaghasi ameshinda kwa kura 2,708 na kufuatiwa na Mathias Zebedayo wa Chadema aliyepata kura 1,455 huku Issa Ally wa UPDP akipata kura 83.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Bryceson Kibassa amesema mgombea wa CCM kata ya Masakta, Martini Kia ameshinda kwa kupata kura 1,489.

 

“Mgombea wa Chadema, Theophil Lolo amepata kura 553. Katika uchaguzi wa kata hii watu 3,483 walijiandikisha kupiga kura,” amesema Kibassa.

 

Amesema kata ya Gehandu mgombea wa CCM, Mathayo Samhenda ameshinda kwa kupata kura 2,252 sawa na asilimia 98.8 ya kura zilizopigwa.

Kibassa amesema mgombea wa ACT-Wazalendo, Daudi Gidabayda amepata kura 21 na Philip Malo wa Chadema amepata kura sita.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga amesema wagombea wa CCM wa kata za Tumati na Hayderery walipita bila kupingwa.

"Mgombea wa CCM kata ya Hayderery, Justin Masuja ameshinda baada ya mgombea wa Chadema, Daniel Homa kujitoa na kata ya Tumati mgombea wa CCM,  Paulo Axweso ameshinda baada ya mgombea wa Chadema, Zacharia Hhaynihhi kuondolewa sababu ya fomu yake ya kugombea kuwa na dosari," amesema.

Awali, washindi hao wote watano walikuwa madiwani wa kata hizo kwa tiketi za Chadema na ACT lakini walijiuzulu na kuhamia CCM ambako walipitishwa kuwania tena nafasi hizo na kushinda.

Chanzo: mwananchi.co.tz