Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM, wasomi wataja siri ya ushindi

17921 Pic+ccm TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku moja baada ya CCM kunyakua ushindi katika majimbo mawili na kata 23 katika uchaguzi mdogo, wasomi na wanasiasa wameeleza sababu za ushindi kuelekea kwa chama tawala pekee tangu Uchaguzi Mkuu 2015.

Uchaguzi huo uliofanyika juzi, ulihusisha majimbo ya Ukonga jijini Dar es Salaam na Monduli mkoani Arusha baada ya waliokuwa wabunge wa majimbo hayo kupitia Chadema kujiunga na CCM na wote kushinda tena.

Wakati Dk Richard Mbunda wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akitoa sababu tatu za chama hicho kushinda kila mara, CCM imetamba kwamba ni kazi nzuri ya Rais John Magufuli.

Hata hivyo, Chadema imedai kwamba hakukuwa na uchaguzi huru unaofuata sheria, kanuni na misingi ya kidemokrasia.

Tangu kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015, zimefanyika chaguzi ndogo mara tano katika majimbo na kata mbalimbali ambazo CCM imeshinda zote, isipokuwa Kata ya Ibigi mkoani Mbeya iliyochukuliwa na Chadema.

Kukusanya nguvu

Kutokana na matokeo hayo, Dk Mbunda alisema ushindi huo wa CCM unatokana na kuhamishia nguvu zote katika sehemu moja tofauti na kipindi cha Uchaguzi Mkuu.

“Hakuna asiyejua kwamba CCM ni chama kikubwa, hivyo kina resources (rasilimali) kubwa ya watu, ndiyo maana unaona katika chaguzi ndogo wanapeleka viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge, mawaziri, katibu mkuu na makada mbalimbali ili kuhakikisha wanawafikia wapigakura wote,” alisema Dk Mbunda.

Msomi huyo wa masuala ya siasa, alisema hata fedha zinazotumika katika uchaguzi huo kwa upande wa CCM haziwezi kulinganishwa na zile zinazotumika kwa vyama vya upinzani.

“Ni rahisi sana kuwekeza katika eneo moja kuliko kipindi cha Uchaguzi Mkuu, fedha hizo inabidi zigawanywe kwa nchi nzima.”

Alisema kuwa katika chaguzi hizo kuna fedha zinazotumika kihalali, ingawa pia haijulikani kiasi gani zinazopita chini ya kapeti, zote zikiwa na lengo la kukisaidia chama kuibuka na ushindi.

Pia, Dk Mbunda alizungumzia alichokiita “upepo wa Magufuli uliopo sasa” hasa vijijini ambako kuna wapiga kura wengi ikilinganishwa na wale wa mijini.

“Hata mijini nako naona wapiga kura ni watu wa kawaida ambao hawatumii mitandao ya kijamii, mfano mzuri tangu chaguzi hizi ndogo zianze idadi ya wapiga kura inapungua kila kukicha, hii ina maana kwamba watu wanaopiga kura ni wa kawaida na wale wa maofisini wanaishia kulalamika tu katika mitandao ya kijamii.”

Alisema hali hiyo inaonyesha kuwa hiki ni kipindi kigumu kwa wapinzani na lazima lifanyike jambo ili kuondoka katika hali hiyo.

“Sasa tunashuhudia unofficial burn (zuio lisilo rasmi) kwa vyama vya upinzani kufanya siasa, hii ndiyo chimbuko la haya yote,” alisema.

Alisema kutokana na zuio hilo wapinzani wanajikuta wanaingia katika uchaguzi bila kujiandaa na kuishia kupata kipindi cha mwezi mmoja kujinadi.

“Huwezi kukatazwa kufanya siasa kipindi chote halafu ukategemea mwezi mmoja utangaze sera zako wapigakura wakuelewe na kukuamini, kama wataendelea hivi tusitarajie miujiza,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Dk Mbunda, hali hiyo inasababisha athari hasi kwa vyama vya upinzani na itafika hatua vyama hivyo vitapotea.

Furaha ya CCM

Wakati mhadhiri huyo akisema hayo, katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema ushindi walioupata ni matokeo ya kazi nzuri ya Rais John Magufuli.

“Rais wetu ambaye ni mwenyekiti wa chama amefanya kazi kubwa na kudhihirika kwa matokeo chanya, ndiyo maana leo tunashuhudia CCM ikishinda,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Polepole, vyama vya upinzani vimeshindwa kutofautisha mambo mazuri na badala yake wameendelea kulaumu kila kukicha hata pale CCM inapofanya vizuri.

“Wanashindwa kutofautisha ni wakati gani wanakosoa au ni wakati upi wanaunga mkono, hakuna mchawi, wanapaswa kujitafakari upya la sivyo wataendelea kulalamika kila kukicha.”

Chadema yalilia haki

Kauli za Polepole zinapingwa na naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu aliyesema ushindi inaoupata CCM unatokana na kutokuwapo uchaguzi wa haki. “Ni kwa sababu hakuna uchaguzi. Chaguzi zinaongozwa na sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi, lakini katika chaguzi hizi hayo yote hayazingatiwi na hakuna anayeheshimu maadili,” alisema.

Aliongeza kuwa, “hapo huwezi sema CCM wameshinda badala yake wameamua kujitengenezea utaratibu wao.”

Mwalimu alisema hiyo ina maana kwamba sasa hakuna demokrasia kwa sababu misingi inayoitengeneza haifuatwi.

“Watawala wamejitia upofu na kufunika kombe kwa kila kinachoendelea sasa, hii inasababisha kuwatia hofu na hasira watu na kusababisha watafakari tofauti,” alisema.

Alisema CCM inajidanganya kwamba inapambana na ufisadi, lakini ukweli ni kwamba imeanzisha ufisadi mwingine wa kukaba demokrasia.

“Wanafikiri kupambana na ufisadi ni kuzuia rushwa na wizi wa mali za umma pekee, ufisadi huu tulionao sasa wa kubaka demokrasia ni mkubwa kuliko wizi na rushwa.”

Mwalimu alionya kuwa kuna siku wananchi watajitambua na kuamka katika shimo.

“Hata paka pamoja na upole wake wote, siku ukimfungia katika chumba na kumuadhibu anageuka kuwa simba kujitetea,” aliongeza.

Mawazo kinzani

Ushindi huo pia ulimuibua mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Peter Michael aliyesema demokrasia ina maana pana na vipengele vingi kama kuwa na uchaguzi huru, utawala wa sheria na la msingi ni kuzingatia wananchi wengi wanataka nini, jambo ambalo Tanzania inajitahidi kufuata.

Alisema sababu ya CCM kushinda chaguzi hizo ni kutekeleza kwa kiasi kikubwa ilani ya uchaguzi waliyoinadi kwa wananchi mwaka 2015.

“Ilani ndiyo inasababisha mtu amchague nani, sasa ilani ya CCM ndiyo inayotekelezwa na mengi yaliyoandikwa yametekelezwa kwa asilimia kubwa, ndiyo maana wapigakura wanaona chama hicho kinafaa,” alisisitiza Dk Michael.

“Unapokuwa mpinzani wewe kazi yako ni kuikosoa Serikali ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana, sasa CCM inatekeleza na upinzani kujikuta hawana cha kukosoa, ndiyo maana wanaona uwepo wao unaanza kufutwa katika macho ya watu.”

Aliunga mkono hoja ya Dk Mbunda kuhusu “upepo wa Magufuli” akisema kwa sasa upepo wa wananchi umehamia kwa Rais Magufuli jambo linalowahakikishia ushindi wa kishindo CCM.

Mhadhiri huyo alisema haoni athari yoyote inayoweza kujitokeza kutokana na ushindi huo kuelekea upande mmoja na kwamba vyama vya upinzani vitaendelea kuwapo, ingawa vinapaswa kubadili namna ya kufanya siasa.

Alisema, “hawatakuwa na kazi tena ya kukosoa, ni muda muafaka sasa wakabadili mtazamo na kuwa na upinzani wa ushirika kama walivyo China.”

“Watu wengi hawafahamu kama China ina upinzani, ina vyama vya upinzani vinane lakini wao hawafuati mfumo wa kimagharibi wa kusutana na kukejeli, badala yake washirikiane na chama tawala ili kutokuwa na madhara.”

Maisha yanaendelea

Akizungumzia uchaguzi wa juzi, aliyekuwa mgombea wa ubunge Chadema katika Jimbo la Ukonga, Asia Msangi alisema hajashtushwa na matokeo ya uchaguzi kwa kuwa dalili zilianza kuonekana mapema asubuhi.

Akizungumza na Mwananchi, Msangi alisema kitendo cha mawakala kuzuiwa kuingia vituoni na mazingira yaliyozunguka uchaguzi huo yalihalalisha ukandamizwaji wa demokrasia.

“Maisha yanaendelea, nawashukuru sana wakazi wa Ukonga wameonyesha kunikubali mno ila mazingira yaliyopo ni kama walivyojionea. Niwape pole kwa yote yaliyotokea tuache kila jambo lina mwisho wake,” alisema.

Aliongeza, “nawasihi wasife moyo, tutafanya kazi kwa kuwa yale yote niliyokuwa nikiwaambia yapo kwenye fremu ya kichwa changu, tutashirikiana kuyafanyia kazi kwa kuwa na mimi ni mkazi wa Ukonga.”

Akizungumzia nini atafanya baada ya matokeo, Msangi alisema, “bado nipo na wanasheria wangu na viongozi wangu wa chama tunaendelea kujadiliana tukifikia uamuzi tutawataarifu.”

Imeandikwa na Tausi Mbowe, Peter Elias na Elizabeth Edward

Chanzo: mwananchi.co.tz