Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimebadili mfumo wa kufanya kampeni kizamani na sasa kitafanya kampeni zake kwa njia ya mtandao ambako kuna wapigakura wengi.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Aprili 12, 2024 na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma Adam Kimbisa na kuungwa mkono na Katibu wa umoja wa vijana wa CCM (UVCCM), Taifa Jokate Mwegelo wakati wa mapokezi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Bara, John Mongella Jijini Dodoma.
Kimbisa amesema chama hicho kimejipanga kufanya kampeni kisasa kwa kutumia mitandao ya kijamii ambako wapigakura ni wengi huko na kuachana na mfumo wa zamani wa kampeni ya nyumba kwa nyumba, mtu kwa mtu, kitanda kwa kitanda na shuka kwa shuka.
"Sasa hivi tunahamia kwenye mtandao ambako kuna kura nyingi huko, tunaondoka kwenye ‘iyena iyena’ tunawafuata hukohuko kwenye mitandao," amesema Kimbisa.
Amesema Mkoa wa Dodoma ndiyo nyumbani kwa CCM, kwani hakuna upinzani na kama inatokea diwani wa upinzani ameshinda hiyo kata, viongozi wa CCM wanakuwa na migogoro lakini kuanzia viongozi wa mitaa, vijiji vitongoji, madiwani na wabunge wote ni wa CCM.
Kimbisa amesema kura nyingi ziko kwa wananchi walioko kwenye matawi, shina na vijiji ambako ndipo CCM itawekeza nguvu kubwa kuwafikia hao kwenye kampeni zao.
Naye katibu wa UVCCM Taifa, Jokate Mwegelo amesema maandalizi ya kufanya kampeni kidijitali yameshakamilika na muda ukifika kazi itaanza rasmi.
Amesema CCM ina vijana wengi wasomi, hivyo itawatumia hao kwenye kampeni zao za mitandaoni, mitaani nchi nzima Tanzania Bara na Visiwani.
"Wanaosubiri vijana tutafanya vibaya nawaambia watasubiri sana maana mwaka huu tumejipanga kushiriki kwenye uchaguzi na niwaambie tu vijana wengi watagombea na nina uhakika tutapata viongozi wazuri kupitia vijana hao," amesema Jokate.
Amesema kitendo cha Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya CCM kumteua na kumthibitisha kwenye nafasi aliyonayo sasa imemfanya ajione ana deni kubwa ambalo anatakiwa alilipe, kwani anajiona ni mwenye bahati kutumikia jumuiya mbili ndani ya CCM.