Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis amesema ziara za Rais Samia Suluhu Hassan nje zisibezwe, kwani zinazidi kuifungua nchi.
Mbali na hilo, pia Mbeto amempongeza Rais kwa juhudi zake za kuimarisha diplomasia inayoongeza fursa za kiuchumi zinazoleta tija na mafanikio kwa pande zote za Muungano.
Mbeto amesema hayo wakati akitoa tathmini na uchambuzi wa fursa na mafanikio ya Tanzania Kimataifa.
Amefafanua kuwa kupitia ziara hizo Rais ameendelea kuipaisha Tanzania kiuchumi ili ifike katika kilele cha maendeleo endelevu, sambamba na kupata hadhi ya nchi iliyoendelea kiuchumi Barani Afrika.
“Uchapakazi wa Rais juhudi, maarifa na ubunifu ndio kibali cha wananchi kumpa ridhaa ya kushinda kwa kishindo Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,”amesema Mbeto.
Kiongozi huyo amewataka wananchi wa visiwa hivyo bila kujali tofauti za kisiasa, kidini na kikabila kumuunga mkono Rais kwa kila hatua anayopiga katika kutafuta fursa mbalimbali kupitia ziara, makongamano na mikutano ya kimataifa.
“Kila mtu ni shahidi kupitia ziara hizo Rais amekuwa akitangaza fursa za utalii kupitia dhana za Royal Tour na uchumi wa buluu zinazofafanua kwa kina rasilimali zilizopo nchini zikiwemo mbuga za wanyama, bahari, mito, maziwa, vivutio vya mambo ya kale ili raia wa kigeni waje kwa wingi nchini kwa ajili ya uwekezaji na utalii.”
“Unaweza kuona thamani ya ziara hizo, si za kifamilia bali anakwenda kutafuta fursa za kiuchumi na kuimarisha mahusiano mema ya kidiplomasia, yakiambatana na kuingia mikataba mikubwa yenye tija kwa nchi,”amesema Mbeto.