Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM: Tunaridhishwa kasi ya Rais Samia

42bb4419298c5caa661d0b6c9f549af1.jpeg CCM: Tunaridhishwa kasi ya Rais Samia

Mon, 3 Jan 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinamuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kasi yake katika kuwatumikia Watanzania kwa kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

Chama hicho kimesema Rais Samia amedhamiria kufungua uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja, jambo ambalo limejidhihirisha kwa vitendo kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, katika dua maalumu ya kumuombea Rais Samia iliyofanyika Magomeni, Dar es Salaam jana.

“Rais Samia Suluhu Hassan ameimarisha na kuboresha mazingira ya biashara nchini hali iliyochochea biashara nyingi kurejea, ikiashiria kuwa hali ya biashara na uwekezaji nchini sasa ni rafiki na wezeshi, alisema.

Shaka alisema Rais Samia ameondoa urasimu katika usajili wa biashara na ameondoa ukusanyaji kodi kwa mabavu, hali ambayo imewafanya Watanzania kuona fahari ya kulipa kodi kwa hiyari.

Katibu huyo wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM alisema kuimarishwa kwa hali ya ufanyajibiashara nchini kumechochea upatikanaji wa manufaa mbalimbali ikiwamo kuongezeka kwa makusanyo ya mapato ya serikali.

Shaka alisema Rais Samia ameonyesha ubunifu na uwezo mkubwa wa kupanga vipaumbele na rasilimali za serikali, pamoja na kuwa makini katika kuhakikisha kila shilingi inayokusanywa, inayozalishwa au inayopatikana inakwenda kuongeza thamani kwenye maendeleo ya nchi na maisha ya Watanzania.

“Ndio sababu tumejionea miradi mikubwa ya kimkakati ikiendelea, miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja ikiendelea, miradi ya maji nayo ikiendelea tena kwa kasi nzuri.”

“Kazi zote hizi na nyinginezo anazofanya Rais Samia ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/25, hivyo Chama kinaridhishwa na kasi yake na kinamuunga mkono kwa asilimia 100,” alisema na kuongeza:

“Kutokana na kasi ya utendaji ya Rais Samia, amewanyima hoja wanaompinga na sasa wameanza kuibua hoja zilizojaa mfumo dume na ubaguzi, hao bu wa kupuuzwa kwani ni hatari kwa taifa.”

Shaka alisema CCM ipo madhubuti, Tanzania ipo imara na salama kwenye mikono ya Rais Samia na kwamba kila kunapoibuka jambo kubwa linalogusa maslahi ya taifa, Watanzania wamekuwa wakiungana pamoja kulinda heshima na maslahi ya nchi.

“Rais Samia ataendelea kufanya mema kwa Watanzania ambayo yatasaidia kuleta maendeleo endelevu kiuchumi, kijamii na kisiasa nchini,” alisema.

Shaka alipongeza kufanyika kwa dua hiyo kwa kuwa Rais Samia anafanya kazi kubwa ambayo inahitaji msaada wa maombi ili afanikiwe zaidi.

“Ninawashukuru sana viongozi wetu wa dini mliotuongozea dua na maombi kwa ajili ya Rais wa nchi yetu, Urais wa nchi ni jukumu kubwa na zito linalolohitaji hekima, busara, afya njema, uadilifu, uzalendo na hofu ya Mungu ili kubeba matumaini na matarajio ya wananchi kwa kuwaongoza kwa haki na usawa pamoja na kuheshimu utawala wa sheria,” alisema.

Akitoa shukrani, Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba aliwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kuwa ni kiongozi aliyejipambanua kupigania maslahi ya wote.

Chanzo: www.habarileo.co.tz