Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM Simanjiro wamkaribisha Millya

21323 USAJILI+PIC TanzaniaWeb

Tue, 9 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Simanjiro. Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Awadhi Omary amemkaribisha aliyekuwa mbunge Simanjiro (Chadema), James Millya ndani ya chama hicho tawala.

Akizungumza leo jioni Jumapili Oktoba 7, 2018, Awadhi amesema hatua hiyo ni faraja kwa CCM hivyo wanamkaribisha kwa mikono miwili kwani jimbo hilo halitakuwa kwenye mikono ya Chadema tena.

Amesema ni jambo la heri kuona mtu akikimbia kwake anakuja kwako endapo atakuja kwa nia nzuri ni furaha kubwa kwako.

Soma zaidi:Lema: Millya alihama siku nyingi Chadema

"Hata hivyo, suala la kugombea ubunge wa Simanjiro litasubiri vikao halali juu ya Millya endapo atapitishwa au laa," amesema Awadhi.

Diwani wa Endiamtu (Chadema), Philemoni Oyogo amesema amesikitishwa mara baada ya kupata taarifa kuwa Millya amejiuzulu nafasi hiyo na amehamia CCM.

Oyogo amesema yeye ataendelea kuwa diwani wa Endiamtu kupitia Chadema na hayupo tayari kujiuzulu nafasi hiyo na kujiunga na CCM.

Diwani wa Mirerani (Chadema), Thomas Yohana amesema hawezi kuzungumza chochote zaidi kwani Millya ametumia demokrasia yake kama Mtanzania kujiunga CCM.

"Siwezi kuzungumza chochote yeye ametumia uamuzi wake ila mimi siwezi kuhama Chadema eti kwa sababu ya kumuunga mkono yeyote nitaendelea kuwa diwani wa Mirerani kwa tiketi ya Chadema," amesema Yohana.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa wilaya ya Simanjiro wamepongeza hatua ya Ole Millya kuondoka Chadema na kujiunga na CCM.

Soma zaidi: Chadema washtushwa taarifa za Millya kujiuzulu

Mkazi wa mtaa wa Kazamoyo, Mustafa Kabota amesema Millya alienda Chadema kwa ajili ya kutafuta mabadiliko lakini amerudi baada ya kuona hakuna mabadiliko yoyote na kuamua kurudi CCM.

"Nawaomba madiwani wa kata ya Mirerani na Endiamtu ambao nao wapo Chadema warudi CCM kwani huko Chadema hakuna wanachokifanya," amesema Kabota.

Mkazi wa Mirerani, Hassan Juma amesema hata ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite uliwekwa ili kuwakomoa wananchi wa eneo hilo baada ya kumchagua Millya na madiwani wa Mirerani na Endiamtu.

"Nadhani sasa hivi tutaruhusiwa kupita ndani ya ukuta kwani haya mambo ya kisiasa yalitugharimu ila kwa sababu jamaa amemuunga mkono mzee sasa mambo yatakuwa safi," amesema Juma.

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Manyara, Gervas Sulle amesema hana taarifa ya Millya kujiuzulu ubunge na kuhamia CCM.

"Sina hizo taarifa rasmi za Millya ila Katiba inamruhusu ni uhuru wa mtu hao wanaosema tumepata pigo hakuna pigo tulilolipata," amesema Sulle.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Millya alimshinda mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka na pia madiwani sita wa Chadema walishinda kwenye kata za Mirerani, Endiamtu, Naberera, Loiborseret, Ruvu Remit na Loiborsoit.

Katika mkoa wa Manyara Chadema ilishinda majimbo mawili ya Simanjiro na Babati Mjini linaoongozwa na Pauline Gekul wa Chadema kati ya majimbo saba.

Soma zaidi: Mbunge wa saba upinzani ahamia CCM

Chanzo: mwananchi.co.tz