Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM Manyara kukutana kumjadili Gekul

Gekul Awataka Wanasheria Kuwasaidia Wananchi Wenye Matatizo Pauline Gekul

Sun, 26 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara kimefanya kikao chake leo Jumapili Novemba 26, 2023 kujadili sakata la Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul anayekabiliwa na tuhuma za ukatili na udhalilishaji, na kesho Novemba 27, 2023 kitatoa tamko lake.

Gekul anatuhumiwa kutoa maelekezo kwa kundi la vijana wake kumwingizia chupa mfanyakazi wake, Hashim Ally au kumpiga risasi kwa madai kwamba alitumwa kimkakati kwenda kwenye hoteli yake ya Paleii Lake View Garden.

Sakata hilo liliibuka baada ya video kusambaa mitandaoni ikimwonyesha Hashim akieleza jinsi alivyofanyiwa ukatili huo na Gekul ambaye hadi jana, alikuwa ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, kabla ya uteuzi wake kutenguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, jana usiku.

Tukio hilo limewaibua wadau mbalimbali wa haki za binadamu na utawala bora wakitaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya Gekul na kijana aliyefanyiwa unyama huo apate haki yake kama raia wa Tanzania.

Akizungumzia sakata hilo leo Novemba 26, 2023, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Manyara, Peter Toima amesema wako kwenye vikao kwa ajili ya kujadili suala hilo, akiahidi kesho, atafutwe, atakuwa na maelekezo kamili.

“Naomba mtupe nafasi, tutasema, ndio kwanza tunataka kuingia kwenye vikao tulizungumzie hili suala, naomba tuwasiliane kesho,” amesema Toima.

Wakati Toima akieleza hayo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amepongeza hatua ya Rais Samia ya kutengua nafasi ya Gekul, akisema ingawa ni wajibu lakini anapaswa kupewa pongezi kwa kuonyesha uwajibikaji

“Unajua hata nyumbani huwa ni wajibu wetu kupeleka chakula, lakini tukila na kushiba tunamshukuru aliyepika. Kitendo alichokifanya Rais Samia watu wamekifurahia, nikiwemo mimi, sasa isiishie hapa, avuliwe uanachama na ubunge.

“Huyu (Gekul), hafai kuwa mbunge, ingawa kutakuwa na makelele mengi ooh…haijathibitishwa, lakini kitendo cha Naibu Waziri kudhaniwa sio ishara njema,” amesema Lema ambaye aliwahi kufanya kazi na Gekul wakiwa Chadema.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa juzi na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus kuhusu kutenguliwa kwa uteuzi wa Gekul, haikueleza wazi sababu za kutenguliwa kwa uteuzi wake kama Naibu Waziri wa Katiba na Sheria.

Usikose kufuatilia gazeti la Mwananchi, tovuti na mitandao ya kijamii ya Mwananchi kwa taarifa zaidi kuhusu sakata hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live