Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM: Katiba isitekwe na wanasiasa

SHAKA 1 1000x640.jpeg Katiba isitekwe na wanasiasa

Thu, 7 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hoja ya Katiba mpya hivi sasa ndiyo imetawala mijadala mbalimbali hasa baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kuiagiza Serikali kuangalia namna ya kufufua mchakato huo uliokwama mwaka 2014 ukiwa katika Katiba Inayopendekezwa inayosubiri kura ya maoni.

Mchakato huo ulianza mwaka 2011 baada ya Rais Jakaya Kikwete kuuanzisha, tangu wakati huo hadi mwaka 2014 CCM imekuwa ikibebeshwa lawama za kuuharibu kwa kutumia Bunge Maalumu la Katiba, hata hivyo chama hicho pia kimekuwa kikikana tuhuma hizo na kudai utashi wa kisiasa ulikosekana kwa baadhi ya walioshiriki.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano baina ya gazeti la Mwananchi na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Shaka Hamdu Shaka

Mwandishi: Kitu gani kimeifanya CCM ikubali hoja ya mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikisemwa kila mara na wapinzani?

Shaka: Hoja ya Katiba mpya si ya wanasiasa na haipaswi kutekwa nao, hii ni hoja yenye masilahi kwa taifa, hivyo kila mwananchi anapaswa kushirikishwa kwa kupewa elimu ili atakapoamua awe na uelewa mpana.

Sisi ndio vinara wa mabadiliko na mageuzi tunayaona katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Huwezi kuogopa wala kusema tumedandia hoja ya watu fulani lakini tunatathmini mchango wa kila mtu bila kujali itikadi yake.

Kwa kuwa tumeshaitaka Serikali ifufue mchakato huo, ni vema tukaiachia jukumu hilo lakini tusiache kuelimishana namna bora ya kuendelea na mchakato huu.

Chaguzi za ndani

Swali: CCM sasa kinafanya chaguzi ambazo nyingine zimefutwa kutokana na hitilafu kadhaa, ikiwemo kupanga safu za uongozi, ni hatua gani umewachukulia wahusika?

Shaka: Kwa asilimia 95 chaguzi hizo za ndani zinakwenda vizuri na wachache wenye michezo michafu wanashughulikiwa kulingana na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa chaguzi hizo, hawatabaki salama

Chama cha siasa kina watu wa aina mbalimbali, wapo wanaoweza kufanya chochote kusaka madaraka. Suala la kupanga safu lipo, kutengeneza makundi, wanaovuruga chaguzi kwa masilahi yao wapo na mambo mengine ya ovyo, ila msingi wa chama chetu ni Katiba, kanuni na taratibu.

Niwaeleze wazi kuwa chama hakitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kukiuka taratibu za uchaguzi, katiba ya CCM imejipambanua vizuri kabisa na kueleza atakayevuruga uchaguzi nini kitamtokea. Katiba hii ndiyo imezaa kanuni za uongozi na maadili, nazo zimeweka wazi kabisa, sasa wewe fanya vurugu zako ila tambua kuna sehemu utakwama.

Tunajua baadhi ya watu wanapanga safu za kuelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, tulishakataza upangaji safu.

Yapo maeneo tumesitisha uchaguzi, yapo maeneo matokeo yamefutwa kabisa, wapo viongozi wameitwa kwenye vikao na adhabu zinatolewa, lengo likiwa kuondoa sintofahamu katika ngazi hizi na kuwapata watu wanaostahili.

Chaguzi za 2024-2025

Mwandishi: Mwaka 2019 na 2020 kulikuwa na malalamiko ya wapinzani kuenguliwa kwa hila katika kuwania uongozi na wagombea wa CCM kupita bila kupigwa, mmejipanga vipi kuondoa kasoro zilizojitokeza

Shaka: Mazingira ya sasa ni tofauti na wakati ule, hata kiongozi wa sasa ni tofauti, lakini nawahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utakuwa bora zaidi kuliko zilizowahi kufanyika huko nyuma.

Rais Samia ana nia ya dhati katika kuliunganisha taifa, hii inatoa taswira chanya kuelekea chaguzi zijazo na kama ilivyo historia ya CCM, hatuna sababu ya kuogopa chaguzi, haswa tuna kiongozi jasiri.

Tunachofanya ni kuhakikisha tunaboresha mazingira ya ufanyaji siasa ili umoja tunaotengeneza uwe na tija, tunawashauri na wenzetu wajifunze namna CCM inavyofanya siasa zake hadi ikaaminika kwa wananchi ili ikifika wakati wa uchaguzi wawe na watu wazuri kwenye kinyang’anyiro.

Mwandishi: Kilio cha wapinzani ni mazingira magumu ya kufanya siasa, ikiwemo mikutano ya hadhara na shughuli zao kuzuiwa, hili mmeliangaliaje?

Shaka: Hali ya siasa za ndani inazidi kuimarika na itakuwa bora zaidi kadiri siku zinavyokwenda huku kukiwa na taswira chanya ya matokeo ya maridhiano kati ya CCM na vyama vingine.

Chini ya utawala wa Samia mtashuhudia mengi mazuri kwenye siasa, amekuwa kinara wa kutaka kuliweka taifa pamoja na ndiyo maana haya mazungumzo yanayaendelea na kama Watanzania hawafahamu vyema niwaeleze kuwa yapo katika hatua nzuri.

Hivi sasa wapinzani wanafanya mikutano kama tunavyofanya sisi, mimi siku chache zilizopita nilikuwa kule Lindi na nimeona wenzetu wa ACT-Wazalendo nao wamefanya bila kubughudhiwa wala kudhuriwa na pia nimeona Chadema wanajiandaa kufanya mikutano ya ndani.

Mwandishi: Kuna baadhi ya makada tayari wanafanya harakati za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, je, mtatoa fumu moja ya urais?

Shaka: Kwa sasa hatuna mawazo hayo kwa kuwa tayari Rais Samia ana sifa za kutuvusha, CCM tuna katiba, kanuni, taratibu na utamaduni na kwa kipindi tulichonacho wala hatuhangaiki kujiuliza itakuwaje kwa sababu kwanza tuna kazi ya kujenga nchi na kuhakikisha ilani ya uchaguzi inatekelezwa na bahati nzuri tunaye jasiri mpambanaji ambaye anatekeleza hii ilani.

Ukimtathmini anatosha kabisa kutuvusha katika nyakati zote tunazokwenda huko mbele, wala hakuna sababu ya kusema tuanze kufikiria. Hilo liko wazi kabisa, jasiri mpambanaji ni mmoja na sisi tunamuombea dua kama ambavyo ameanza vizuri, basi atakamilisha vizuri kuelekea 2030, hatutafuti mgombea kwa kuwa anayefanya kazi nzuri yupo.

Mikutano ya hadhara

Mwandishi: Wapinzani wanalalamika kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara, lakini ninyi mnaifanya, hamuoni mnatengeneza ubaguzi?

Shaka: Hatufanyi mikutano ya hadhara, tunachofanya CCM ni ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na vikao vya ndani ambavyo hata vyama vingine vinafanya.

Sisi tuna jukumu la kusimamia utekelezaji wa ilantuliyoinadi wakati tukiomba kura mwaka 2019 na 2020, kila baada ya miezi mitatu na sita kuna vikao vya kutathmini utekelezaji huo, hivyo lazima tukague ili tuone ni kwa namna gani tumefanikiwa au kuna changamoto gani.

Suala la watu kukusanyika kumpokea kiongozi ni jingine, maana wana CCM hawawezi kumuacha kiongozi apite bila kumpokea, huwezi kuwazuia hasa pale wanapoona mazuri yaliyofanyika, hiyo sio mikutano ya hadhara ni mapokezi.

Mapokezi ya aina hiyo hata wenzetu huwa wanapokewa wakienda huko kwa wananchi, tofauti yetu ni kuwa sisi ni wakubwa tuna wafuasi wengi lakini wao ndiyo wanakua.

Uimara wa Bunge

Mwandishi: Wapo wanaoona Bunge la sasa haliiwajibishi Serikali vilivyo kwa kuwa lina wabunge wengi wa CCM wanaounga mkono hata hoja zisizo na tija, hili unalizungumziaje?

Shaka: Bunge kuwa na wabunge wengi wa CCM hakulifanyi liwe na mawazo ya upande mmoja au kuunga mkono kila kinachopelekwa na Serikali, kinachoangaliwa ni uwezo wabunge na hoja wanazoziwasilisha zimebeba masilahi ya wananchi na Taifa.

Tumeshuhudia mjadala wa bajeti wabunge wetu wamedadavua vizuri na wametoa mwelekeo kwa kuishauri Serikali vizuri na hata kuna maeneo yamefanyiwa marekebisho kutokana na michango ya wabunge. Ni wakati sasa wenzetu wanatakiwa kujifunza kwa namna gani CCM tunafanya mambo yetu ili iwaandae watu wazuri tukutane kwenye kueleza sera zetu kwa wananchi ambao ndio waamuzi.

Pia nimesikia madai kuwa kuna upendeleo bungeni, sisi hatulioni hilo na tunaamini kule zinachaakatwa hoja kutoka kwa wawakilishi ambao wanazingatia masilahi ya umma.

Naamini itikadi za kisiasa zisipowekwa mbele katika mijadala yenye tija, tutakuwa na Taifa bora.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live