Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM, Chadema wazungumzia Serikali ya Finland kujiuzulu

CCM, Chadema wazungumzia Serikali ya Finland kujiuzulu

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Viongozi wa CCM na Chadema wametoa maoni yanayofanana kuhusu uamuzi wa Serikali ya Finland kujiuzulu baada ya kushindwa kutimiza ahadi yake ya kufanya mabadiliko ili kuboresha mfumo wa afya na hifadhi ya jamii.

Ijumaa iliyopita, aliyekuwa Waziri Mkuu, Juha Sipila ambaye alikuwa anaongoza serikali ya mrengo wa kulia, aliwasilisha barua ya kujiuzulu baada ya kushindwa kusukuma mabadiliko hayo, ikiwa ni wiki tano kabla ya uchaguzi wa wabunge.

Awali, kulikuwa na juhudi za kutaka kufanya mabadiliko hayo kwa takriban miaka 10.

Wakati akiingia, Sipila alieleza kushindwa kufanya mabadiliko hayo kuwa ni fedheha.

Tangu mwaka 2015, Sipila ameongoza serikali ya umoja inayoundwa na chama chake cha Centre Party, Muungano wa Kitaifa (National Coalition) na chama cha mabadiliko ya bluu (Blue Reform). Vyama hivyo havikuweza kukubaliana na mapendekezo yaliyowasilishwa na Sipila ambayo aliyapa kipaumbele. Mara kwa mara alikuwa akitishia kujiuzulu kama mabadiliko hayo yasingefanikiwa.

Mabadiliko hayo yalilenga kupunguza gharama zinazopaa za matibabu ya wazee ambao wanaongezeka kwa kasi. Kiwango cha watu wenye umri wa miaka zaidi ya 65 kwenye nchi hiyo ya Nordic yenye watu milioni 5.4 kinatarajiwa kufikia asilimia 26 ya watu wote ifikapo mwaka 2030.

Kutokana na hali hiyo, serikali ilipendekeza shughuli zote za matibabu zifanywe katika ngazi ya mkoa badala ya manispaa na matumizi ya watoa huduma wa afya wa sekta binafsi, kitu kilichoibua mjadala mkubwa.

Lakini vyama hivyo vikashindwa kukubaliana katika mambo kadhaa ikiwamo ni kwa kiasi gani mfumo huo utakuwa wazi kumuwezesha mgonjwa kuwa huru kuchagua huduma.

Mzozo huo ulisababisha Sipila awasilishe barua kwa rais akieleza kuwa serikali yake imejiuzulu.

Alipoulizwa maoni yake kuhusu uamuzi huo wa serikali ya Finland kujiuzulu, Kanali Ngemela Lubinga, ambaye ni katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM anayeshughulikia uhusiano wa kimataifa, alisema ulifikiwa kwa kuwa waliona hawajatimiza walichoahidi.

“Na taratatibu zao zinaruhusu,” alisema Lubinga.

“Wenzetu wanakula kiapo na wameona walichotarajia hawakutimiza ndio maana wameamua kuachia ngazi. Si jambo la ajabu. Hata huku lilishawahi kutokea.” Hata hivyo, Kanali Lubinga hakutaka kufafanua lililowahi kutokea Tanzania.

Kwa upande wake, katibu mkuu Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema uamuzi huo ni hatua kubwa ya binadamu kujitambua.

“Kwa sababu huwezi kung’ang’ania cheo au madaraka wakati jukumu ulilopewa hukulitimiza ipasavyo,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz