Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM, Chadema uso kwa uso uzinduzi wa barabara Dar

32349 Usopic Tanzania Web Photo

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Unaweza kusema hafla ya uwekaji jiwe la msingi la upanuzi wa barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam umewakutanisha wanachama wa CCM na Chadema.

Wanachama hao wakiwa wamevalia sare za vyama vyao wamejitokeza kwa wingi leo Jumatano Desemba 19, 2018 kushiriki hafla hiyo inayofanyika eneo la Kimara Stop Over huku wakiwa wameketi pamoja.

Si kila mmoja kuvaa sare za chama chake, pia baadhi walionekana kuimba na kutabasamu ili mradi tu kufurahia tukio hilo.

Wakati wanachama wa CCM wakiimba nyimbo za chama hicho, wa Chadema wameonekana wakinyoosha mikono juu na kuonyesha vidole viwili ishara inayotumiwa na chama chao huku wakiwa na baadhi ya wanachama wa CUF.

Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika naye ni miongoni mwa waliojitokeza katika uzinduzi huo na kuketi sambamba na mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia. Awali Mtulia alikuwa mbunge wa Kinondoni kwa tiketi ya CUF.

Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara ambaye awali alikuwa mbunge wa Ukonga kwa tiketi ya Chadema kabla ya kuhamia CCM na kupitishwa kuwania ubunge na baadaye kuteuliwa kuwa naibu waziri, naye amehudhuria hafla hiyo na ameonekana akisalimiana kwa bashasha na Mnyika.

Rais John Magufuli ndiye atakayeweka jiwe la msingi la upanuzi wa barabara hiyo ambayo leo kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana imefungwa kuanzia eneo la Kimara Stop Over hadi Kimara Temboni.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 19.2 kutoka Kimara hadi Kibaha ikikamilika itakuwa na njia nane.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni waliokuwa wenyeviti wa CCM wa mikoa na wilaya ambao jana Halmashauri Kuu ya chama hicho tawala ilitangaza kuwasamehe na kuwarejeshea uanachama wao wakiwemo Ramadhan Madabida na Salum Madenge.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz