Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM Arusha wajipanga kujaza nafasi zilizo wazi

47f7b908b949229c328242f6fc7ead11 CCM Arusha wajipanga kujaza nafasi zilizo wazi

Tue, 9 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arusha kimeawaagiza makatibu wa chama hicho ngazi za kata na matawi kuanzia leo kutoa fomu kwa wanachama wanaotaka kujaza nafasi zilizo wazi.

Agizo hilo lilitolewa juzi na Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha, Denis Mwita kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 44 ya CCM yaliyofanyika eneo la Kilombero, kata ya Levolosi.

Aliwataka viongozi hao kutokuweka mizengwe kwa wanachama ambao watachukua fomu za kugombea uongozi ndani ya chama kujaza nafasi zilizoachwa wazi na baadhi ya waliokuwa kwenye uongozi kupata nafasi nyingine za uongozi katika uchaguzi mkuu uliopita.

“Kuweka mizengwe ni kwenda kinyume na mwongozo wa chama hivyo viongozi hao wahakikishe utoaji wa fomu unafanyika kwa uwazi bila mizengwe au upendeleo wa aina yoyote na tayari maelekezo pamoja na ratiba ya uchaguzi mdogo ndani ya chama yameshatolewa,” alisema.

Mwita aliwataka wanachama wa CCM wafanye kazi za halali kwani ujanjaujanja hauna nafasi ndani ya chama.

Aidha, aliwaonya wanaotumia mavazi ya chama, nembo ya chama, bendera na sare kujipatia maslahi binafsi kuacha mara moja na akawaomba wananchi kutoa taarifa ili kuwabaini watu wa aina hiyo.

“Sare na nembo za CCM zisitumike kama kichaka bali zitumike kuondoa kero za wananchi kwa kuwa chama kimejengwa katika misingi yake imara na sio ujanjaujanja.”

“Chama kimeshaikabidhi serikali Ilani ya uchaguzi hivyo inapaswa kuitekeleza ipasavyo kwa kuwa huo ndio mkataba kati ya chama na wananchi,” alisema.

Katibu huyo wa CCM wilaya ya Arusha alisema baada ya uchaguzi chama na jumuiya zake zimefungua milango kwa wananchi wanaotaka kujiunga, lengo likiwa ni kujenga uhai wa chama na jumuiya zake kwa kuongeza idadi ya wanachama.

Alisema wakati wa maadhimisho ya miaka 44 ya CCM, chama na jumuiya zake kimefanya shughuli mbalimbali za kujitolea ikiwamo kushiriki ujenzi wa shule za sekondari na msingi, usafi kwenye masoko, kutembelea vituo vya watoto na kuwapatia misaada.

“Pia tulitembelea viwanda ili kuangalia utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na kutoa damu kwa ajili ya wagonjwa hospitali huku Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wakiendesha darasa la itikadi kwa vijana wenzao,” alisema.

Aliwahakikishia wananchi kwamba ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu katika jiji la Arusha zitatekelezwa kupitia madiwani wa halmashauri ya jiji pamoja na na Mbunge wa jimbo na wabunge viti maalumu .

Chanzo: habarileo.co.tz