Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM: Acheni kumshinikiza Rais Samia

359348f42abcbfe253ca4a50471626b8.jpeg CCM: Acheni kumshinikiza Rais Samia

Mon, 14 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakuna chama cha siasa chenye wajibu wala haki ya kumshinikiza Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Samia Suluhu Hassan kuhusu muda, wakati na namna ya kuwaona wananchi.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wazee wa wilaya ya Muheza mkoani Tanga jana.

Alisema baadhi ya matamko ya viongozi wa upinzani hayana afya katika ujenzi wa umoja wa kitaifa kwani amejipambanua kuwatumikia Watanzania bila kuwabagua.

“Matamshi yaliyotamkwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa hivi karibuni yamevuka mipaka huku yakiwathibitishia Watanzania kuwa baadhi ya vyama hivyo hakuna wanasiasa wenye maarifa na upeo wa kutambua dhana ya mgawanyo wa madaraka,” alisema.

Shaka alisema wapo viongozi wa vyama vya upinzani ambao wamekuwa mahiri wa kuzusha mambo, kupotosha, kuchochea chuki lakini kamwe hawatafanikiwa.

“Hakuna sababu ya kutishana wala kutoa masharti na shinikizo kwa jambo lolote lile kwani Rais Samia kwa kuthamini kwake ushirikishwaji wa kila mmoja wetu katika ujenzi wa nchi yetu akaona inafaa kukutana na vyama vya siasa, hivyo ataamua ni wakati gani akutane nao na kamwe wasitake kuharibu nia hiyo njema ya Rais,” alisema.

Shaka alisema CCM itaendelea kutoa mwelekeo wa siasa na uongozi wa nchi kwa kuwa ndio chama kinachounda serikali, hivyo viongozi wa chama hicho kwenye ngazi zote wana jukumu la kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya 2020-2025.

Alisema CCM haitashiriki siasa za kisasi au kuwagawa wananchi kwa sababu ina mwelekeo wa siasa safi zinazojali ustawi wa haki, usawa, amani, usalama, umoja na mshikamano na kusimamia maslahi ya wananchi.

Shaka yuko katika ziara ya kikazi mkoani Tanga ambapo ataendelea na ziara yake katika wilaya ya Tanga Mjini.

Ziara hiyo inaongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ambaye tayari amefanya ziara katika wilaya za Kilindi, Handeni na Korogwe.

Katika ziara hiyo, Chongolo ameongozana pia na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Kanali mstaafu, Ngemela Lubinga ambaye anapita wilaya za Mkinga, Lushoto na Bumbuli

Chanzo: www.habarileo.co.tz