CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua kampeni za uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Ushetu wilayani Kahama,mkoa wa Shinyanga kwa kuwaomba wananchi wamchague mgombea kupitia chama hicho, Emmanuel Cherehani.
Naibu Katibu Mkuu CCM taifa, Christina Mndeme alizindua kampeni hizo kwa kumuombea kura Cherehani ili aendeleze aliyoyaacha mtangulizi wake, Elias Kwandikwa aliyefariki dunia.
Mndeme alizindua kampeni hizo kwenye kata ya Nyamilangano na kumnadi mgombea huyo kuwa anazifahamu changamoto za jimbo hilo na amekuwa kiongozi wa muda mrefu kwenye ushirika.
"Ni mwenyekiti wa chama cha wakulima wa zao la tumbaku, amekuwa kiongozi wa mfano nchini kwa kuongoza chama cha ushirika (Kacu) vizuri hivyo tukimpa kura atasimamia vyema mazao ya pamba na tumbaku na atasimamia vyema maendeleo yetu tumpeni kura," alisema.
Mndeme alisema Cherehani atasimamia suala la umeme katika kata 20 ambazo hazina huduma hiyo na mkandarasi amepatikana na pia atasimamia upatikanaji maji.
Kwa upande wake, Katibu wa Siasa Idara ya Oganaizesheni Taifa wa CCM, Dk Moulding Castico alisema chama hicho kinawezesha wananchi kupata maendeleo na nchi kuendelea hivyo akaomba wananchi wa jimbo hilo wamchague Cherehani awe mbunge wao.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa alisema watahakikisha mgombea huyo anapata ushindi na wamejipanga kuwasimamia wananchi kutatua changamoto zinazowakabili.
Cherehani aliwaomba wananchi wamchague na akaahidi atatekeleza wajibu wake bila ubaguzi wa aina yoyote. Alitaja baadhi ya mambo atakayosimamia kuwa ni ubora wa barabara, miradi ya maji, huduma za afya na kilimo.
Wakati huohuo, mgombea wa chama cha ACT-Wazalendo Jimbo la Ushetu, Mabula Julius amewaomba wananchi wa jimbo hilo wamchague ili asimamie na kumaliza changamoto kwenye kilimo hasa zao la pamba na tumbaku.
Alisema hayo kwenye uzinduzi wa kampeni za chama hicho kwenye kata ya Ulowa.
Alisema wakulima kwenye jimbo hilo wamesahaulika hivyo wakimchagua atahakikisha analeta maendeleo kwa kuisimamia serikali waweze kupata haki.
"Wananchi wa Jimbo la Ushetu asilimia 100 ni wakulima na dhahabu yao ni mazao, hivyo nitashughulikia pia nitauunganisha miundombinu ya barabara kwenye kata ambazo hazipitiki kirahisi na wakulima kusafirisha mazao yao kwa tabu," alisema Julius.
Alisema bado kuna changamoto ya uhaba wa maji na nishati ya umeme hivyo atahakikisha wananchi wanapata umeme ili waweze kufanyakazi za uzalishaji kwa kutumia umeme na kuongeza vipato.
Uchaguzi mdogo Jimbo la Uchetu utafanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo kupitia CCM, Elias Kwandikwa aliyefariki dunia hivi karibuni.