Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM, ACT-Wazalendo wapigana kumbo Pandani

E4770655ea40061e1ed276c8608bcdc0.jpeg CCM, ACT-Wazalendo wapigana kumbo Pandani

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VYAMA vya CCM na ACT-Wazalendo vimezindua kampeni za Uchaguzi Mdogo katika Jimbo la Pandani Mkoa wa Kaskazini Pemba na kuahidi kufanya kampeni zenye lengo la kudumisha maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa kwa ajili ya amani na utulivu.

Akizindua kampeni za Chama Cha Mapinduzi, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Dk Juma Abdallah Sadalla aliahidi ushindi katika uchaguzi huo na kuwa kampeni hizo zitafanyika kwa kuzingatia na kudumisha maridhiano ya kisiasa.

Aliwataka wananchi wa Jimbo la Pandani kujenga imani kwa CCM ambayo siku zote ikiahidi hutekeleza ahadi zake kwa vitendo.

“Kampeni zitakuwa za aina yake zikifanyika kwa kuzingatia maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa na vyama vyetu kwa lengo la kujenga amani na utulivu uliopo sasa,” alisema Dk Sadalla.

Mwenyekiti wa CCM Pandani, Siasa Khamis alisema CCM ndiyo yenye uwezo wa kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo, hivyo kamwe wasifanye makosa ya kutokichagua kwani kina uzoefu wa kuleta maendeleo.

“'Wananchi wa Jimbo la Pandani msifanye makosa, kichagueni Chama Cha Mapinduzi ili kiwaleteeni maendeleo na kukidhi malengo na matarajio yenu,” alisema Khamis.

Mgombea wa nafasi ya uwakilishi wa Jimbo la Pandani kwa tiketi ya CCM, Mohamed Juma Ali ameahidi kufanya kampeni za kistaarabu zenye kuzingatia maridhiano ya kisiasa kwa ajili ya kudumisha amani na utulivu.

“Nichagueni ili niwatumikie na kuleta maendeleo ya Jimbo la Pandani kwa maslahi ya wananchi wake,” alisema Ali.

Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto aliwataka wananchi wa Jimbo la Pandani katika njia bora zaidi ya kumuezi Maalim Seif Sharif Hamad ni kumchagua mgombea wa jimbo hilo kwa tiketi ya chama hicho.

Zitto alisema hayo katika uwanja wa mpira Kiungoni katika uzinduzi wa kampeni za mgombea wa uwakilishi jimbo hilo, Profesa Omar Faki Hamad na kusema Maalim Seif alikuwa mzalendo na muumini wa dhati wa maridhiano ya kisiasa huku siku zote akiona Wazanzibari wanapiga hatua kubwa ya maendeleo.

“Wananchi wa Jimbo la Pandani mchagueni mwenzenu Profesa Omar Faki Hamad awe mwakilishi wa jimbo hili akawatumikie ndani ya Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kuleta maendeleo...huyu alikuwa rafiki mkubwa wa Maalim Seif Sharif Hamad,” alisema Zitto.

Awali Profesa Hamad aliwaomba wapigakura wa jimbo hilo wajitokeze kupiga kura na kumwezesha kuwasilisha vilio vyao katika Baraza la Wawakilishi.

“Nichagueni ili nitimize ndoto zenu za kuleta maendeleo katika Jimbo la Pandani, hatua ambayo itakuwa tunatekeleza kwa vitendo kauli za kumuenzi mwenyekiti wetu wa chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad,” alisema Profesa Hamad.

Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Pandani unafanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mwakilishi mteule, Abubakar Khamis Bakary kutoka ACT-Wazalendo kufariki dunia Novemba mwaka jana.

Chanzo: www.habarileo.co.tz