Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bunge latoa siku 60 marekebisho sheria ndogo

Bunge La Tanzania Bunge latoa siku 60 marekebisho sheria ndogo

Thu, 9 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

BUNGE limeelezwa kuwa baadhi ya sheria ndogo zina dosari na limetoa siku 60 zirekebishwe.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, Dk Jasson Rweikiza alisema Bunge linaazimia kwamba, mamlaka zilizotunga sheria ndogo zenye kukinzana na masharti ya Sheria Mama na sheria nyingine za nchi zirekebishe sheria ndogo hizo ndani ya siku 60 ili kuondoa dosari hiyo.

Dk Rweikiza alisema hayo bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha taarifa ya mwaka ya shughuli za kamati hiyo kwa kipindi cha Februari mwaka jana hadi Januari mwaka huu.

“Bunge linaazimia kwamba, mamlaka zilizotunga sheria ndogo zilizokutwa na dosari ya kutozingatia misingi ya uandishi bora wa sheria, zirekebishe dosari hiyo ndani ya sitini kuanzia leo (jana) ili kuleta tija kwa watumiaji wa sheria hizo,” alisema.

Pia Dk Rweikiza alisema Bunge linaazimia kwamba, mamlaka zinazotunga sheria ndogo zilizobainika kuwa na masharti yasiyozingatia uhalisia, zifanye marekebisho ndani ya siku sitini kuanzia leo (jana), ili kuendana na uhalisia na kurahisisha utekelezaji wake.

“Bunge linaazimia kwamba, mamlaka zilizobainika kutotekeleza maazimio ya Bunge zitekeleze maazimio hayo ndani ya siku thelathini kuanzia leo na kuwasilisha taarifa za utekelezaji wake wakati wa vikao vya Kamati vya mwezi Machi, 2023,” alisema.

Dk Rweikiza aliwaeleza wabunge kuwa sheria ndogo 13 zina masharti yanayokinzana na Katiba na nyingine 10 zina masharti yanayokinzana na sheria mama na sheria nyingine za nchi.

Alilieleza Bunge kuwa sheria ndogo 27 zina makosa ya kutoendana na misingi ya uandishi.

“Makosa hayo nia kama vile kutorejea vifungu sahihi, kurejea vifungu ambavyo havipo, kutokukamilika kwa sheria ndogo kwa kutokuwepo kwa baadhi ya vipengele muhimu vya kisheria ili kukamilisha sheria husika,” alisema Dk Rweikiza.

Alisema sheria ndogo 12 zinaweka masharti yasiyo na uhalisia ambayo yataleta changamoto katika utekelezaji wake na sheria ndogo 15 zina makosa ya maudhui ya majedwali kutofautiana na vifungu vinavyoyaanzisha au makosa ya kutokukamilika kwa majedwali au kuanzishwa kwa majedwali yasiyokuwepo ama kukosekana kwa majedwali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live