Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bunge la Tanzania laitaka Serikali isitishe akaunti ya Escrow

Bunge Picmaeneo 5 Bunge la Tanzania laitaka Serikali isitishe akaunti ya Escrow

Fri, 9 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bunge la Tanzania limeitaka Serikali kusitisha kuanzisha Akaunti Maalumu (Escrow Account) kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi na kutangaza utalii, kwa kuwa inaweza kusababisha fedha za umma kutumika bila usimamizi na uwajibikaji.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava amesema hayo bungeni leo Ijumaa, Februari 8, 2024, wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati yake kwa mwaka 2023.

Amesema mwaka 2023, Bunge liliazimia Serikali ihakikishe Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (Tawa) zinabakia (retain) na asilimia 30 ya makusanyo yao na asilimia 70 inakwenda mfuko mkuu wa Serikali.

Mnzava, ambaye pia ni mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), amesema hali ilivyo sasa, kiasi chote cha makusanyo huenda mfuko mkuu wa Serikali, hivyo taasisi hizo kutegemea fedha za mishahara, matumizi mengineyo (OC) na miradi ya maendeleo kutoka serikalini.

“Hali hii inachangia kuzorota kwa shughuli za taasisi, hasa kwa aina ya kazi zake zinazohitaji fedha haraka ili kuhakikisha zinatengeneza miundombinu yao kukidhi mahitaji ya watalii,” amesema Mnzava.

Pia, amesema Serikali ilieleza kamati yake kuwa imeona umuhimu wa hoja hiyo, hivyo kuanzisha akaunti maalumu itakayokuwa inatoa asilimia sita, ikiwa na maana kuwa asilimia tatu kwa ajili ya uhifadhi na asilimia tatu kwa ajili ya kutangaza utalii kupitia taasisi hizi.

Mwenyekiti huyo amefafanua fedha hizo zitawekwa katika akaunti hiyo na taasisi hizo tatu zitatakiwa kuorodhesha mahitaji yake na kuyapeleka Hazina kwa ajili ya matumizi ya fedha hizo.

Amesema kamati kwenye uchambuzi wake, ilibaini wazo hilo la Serikali linatoa mwanya wa fedha za umma kuchezewa kwa sababu halitokani na mpango wa bajeti, sheria yoyote ile wala ushauri wa Bunge.

Mnzava amesema utaratibu wa kufungua akaunti maalumu hufanyika pale kunapokuwa na mgogoro wa pande mbili kuhusu mgawanyo wa mapato ya fedha zao ambapo huzitunza  katika akaunti hiyo, hadi pale suluhu ya mgogoro huo itakapopatikana.

“Swali la kujiuliza, je, kuna mgogoro wa mgawanyo wa mapato kati ya taasisi hizi na Hazina. Na kama hakuna, kwa nini Hazina waje na wazo hili? Mheshimiwa Spika, fedha zinazokuwa kwenye akaunti hii maalumu hata ukaguzi wa matumizi yake huwa sio wa kawaida,” amesema Mnzava.

Amesema kuanzishwa akaunti ya Escrow, kutasababisha matumizi ya fedha za umma kushindwa kufanyiwa ukaguzi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa utaratibu wa kawaida.

Amesema kamati inaona suluhu pekee ya kushughulika na matatizo ya taasisi hizo za uhifadhi ni kuhakikisha wanabaki na sehemu ya fedha wanazokusanya kwa ajili ya taasisi hizi kujiendesha kwa ufanisi, kwa kuzingatia aina na mazingira ya kazi zao.

Amesema kwa kufanya hivyo, itahakikisha matumizi ya fedha hizo ambazo ni za umma zinakaguliwa na CAG.

“Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia Serikali isitishe mara moja kuanzishwa kwa akaunti hiyo, hali inayoweza kusababisha fedha za umma kutumika bila usimamizi na uwajibikaji,” amesema Mnzava.

Aidha, Bunge limeitaka Serikali ifanye Marekebisho ya Sheria ya Fedha kwa lengo la taasisi hizo kubaki na sehemu ya makusanyo yake (retention), ili kuzisaidia taasisi hizo kutekeleza majukumu yake ya uhifadhi kwa ufanisi.

Malipo ya fidia

Mnzava alipendekeza Serikali ihakikishe kunakuwa na uthibitisho wa uwepo wa fedha za kulipa fidia utakaotolewa na wizara, taasisi au mwekezaji anayekusudia kutwaa ardhi husika.

Amesema hiyo itasaidia kuweka msisitizo kuwa, kama hakuna fedha za kulipa fidia basi suala la utwaaji ardhi lisubiri mpaka fedha za kulipa zitakapokuwepo.

Kuhusu changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, Mnzava pamoja na mambo mengine amelitaka Bunge kuazimia Serikali ihakikishe inafanya marejeo ya Kanuni za Malipo ya Kifuta Machozi au Jasho ya Mwaka 2011 ili kuboresha viwango kwa aliyeathirika na wanyama wakali na waharibifu, ili kuendana na hali maisha ya sasa.

Kwa upande wa migogoro ya ardhi, Mnzava amesema kumekuwa na malalamiko ya kiutendaji kwa kamati ya mawaziri wanane wa kisekta ambayo yameathiri utatuzi wa migogoro katika vijiji na mitaa 975.

Amesema Bunge linaazimia Serikali ihakikishe inakamilisha utekelezaji wa utatuzi wa migogoro na kamati ya mawaziri ishirikishe wananchi na wawakilishi wao, ili kutatua migogoro katika vijiji na mitaa 975 na uwe shirikishi na wa kudumu.

Akichangia Mbunge wa Donge, Soud Mohamed Juma, amesema amesikia Serikali imeanzisha akaunti ya Escrow ambapo asilimia 6 ya makusanyo itawekwa  kwenye akaunti hiyo, huku mgawanyo ukiwa asilimia tatu zitakwenda kwenye uhifadhi na zilizosalia kutangaza utalii.

“Lakini mimi kwangu naona hili sio suluhisho ambalo lina afya. Ningeomba Waziri wa Fedha akafuata maelekezo ya Bunge lako tukufu kwamba twende tukaweke retention (tukabakize) ambayo itakwenda kusaidia hizi hifadhi zetu za Tanapa, Tawa na NCAA,”amesema.

Majibu ya Mawaziri

Akichangia taarifa hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amesema kulikuwa na hoja ya akaunti ya Escrow na kuona ni kwa namna gani taasisi za Tanapa, Tawa na NCAA zitabakiza fedha za makusanyo yao badala ya kwenda mfuko mkuu wa Hazina na baadaye kurudi tena katika taasisi hizo.

Amesema wameendelea kufanya mashauriano na Wizara ya Fedha ili  watakapokuwa wakiandaa Muswada wa Fedha ambao hupelekwa bungeni kila mwaka, waone ni kwa namna gani taasisi hizo zitawezeshwa kubaki na makusanyo yake.

Kairuki amesema kwa kufanya hivyo kutatawezesha taasisi hizo kuzitumia kuendeleza miundombinu na shughuli nyingine zitakazohitajika.

Kuhusu wanyama waharibifu, Kairuki amesema wameendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo, na tathmini inaonyesha wilaya takribani 44 ndizo zilizoathirika nchini.

Amesema wanyamapori wengi wamekuwa wakitoka nje ya hifadhi wakati wa kiangazi kwa lengo la kutafuta maji na hivyo Serikali inaongeza kasi katika uwekezaji wa kuchimba mabwawa, matumizi ya teknolojia, kujenga vituo vya askari na kuongeza idadi ya askari.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda amesema suala la kutatua migogoro ya ardhi wanaendelea nalo na wanatengeneza mifumo.

“Kule kumove (kwenda) kwa mkono bila kutumia mitandao hii mara nyingi imesababisha vitu vingi mara doble allocation (watu zaidi ya mmoja kumilikishwa kiwanja) bila sababu za msingi, sasa dawa inachemka. Niwaombe wabunge hadi Bunge linalokuja tutakuwa tunatoa taarifa ya utekelezaji,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live