Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), wamemchagua Joseph Ntakarutimana kutoka nchini Burundi kuwa Spika wa bunge hilo katika uchaguzi uliofanyika leo Desemba 20 mjini Arusha.
Ntakarutimana ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama tawala nchini Burundi cha (CNDD-FDD) amechukua nafasi ya aliyekuwa spika wa zamani, Martin Ngoga kutoka nchini Rwanda.
Spika huyo amekuwa ni mgombea pekee wa nafasi hiyo baada ya wagombea wawili kutoka nchini Sudani Kusini, Gai Deng na Dk Anne Itto kujitoa dakika za mwisho na hivyo kusababisha mgombea huyo kukosa ushindani.
Akisimamia uchaguzi huo, Katibu wa Bunge la EALA, Alex Obatre ametoa nafasi kwa wagombea hao waliojitoa kutamka kwa vinywa vyao kuwa wamejitoa, baada ya kuwasilisha taarifa rasmi ya kujitoa, ambapo wamesimama na kusema wana muunga mkono mpinzani wao.
Katika upigaji kura Spika huyo mpya amepata kura za ndiyo 54 kati ya kura 63 za wabunge wote kutoka nchi saba za EAC, ambapo kura nane ziliharibika na kura moja haikupigwa kabisa.