Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Doto Biteko amewataka viongozi wa umma kutotumia kivuli cha cha kufuata taratibu kuchelewesha maendeleo nchini.
"Niwaombe viongozi wenzangu tuliopewa dhamana na Mheshimiwa Rais, kuhakikisha tunawahudumia kwa vitendo wananchi na kuinua hali za wanyonge kwa kuwapatia huduma bora wanazostahili kwa wakati," amesema Dk Biteko.
Dk Biteko ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Desemba 29, 2023 wakati wa uzinduzi wa zahanati ya Bungoni, iliyopo jijini Dar es Salaam.
Amesema kuna baadhi ya viongozi wanaojificha kwenye kivuli cha kufuata taratibu, huku kwa makusudi wakichelewesha maendeleo kwa wananchi.
Akizungumzia zahanati hiyo, amesema ina uwezo wa kuhudumia wakazi 12, 000 kutoka katika kata nne zilizopo wilaya ya Ilala ambazo ni Ilala, Buguruni, Sharifu Shamba na Mchikichini.
Ujenzi wa zahanati hiyo ulianza Februari mwaka huu kwa jitihada za wananchi na baadaye kuungwa mkono na Serikali na wadau wa maendeleo (African Relief Agency na Taasisi ya Rahma International kutoka Kuwait). Ujenzi umegharimu Sh351 milioni ukihusisha gharama za ujenzi, samani, dawa na vifaa tiba.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akiteta jambo na mbunge wa Ilala na Naibu Spika Mussa, Azan Zungu Kwenye hafla ya uzinduzi wa zahanati ya Bungoni, jijini Dar es salaam leo.
Kabla ya uzinduzi huo, DkBiteko alitembelea zahati ikihusisha jengo la wagonjwa wa nje (OPD), kliniki ya baba, mama na mtoto pamoja na jengo la kujifungulia na sehemu ya wageni wanaokwenda kusalimia wazazi.
Akizungungumza wakati wa hafla hiyo, Mbunge wa Ilala na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amewataka watendaji kuhakikisha wanatumia vyema fursa za wafadhili wanaokuja kuwekeza kwenye sekta ya afya na kuondoa mikwamo inayochelewesha maendeleo.
Amesema Wilaya ya Ilala inapokea wageni wengi kwa siku, sambamba na wananchi wenye mahitaji kwenye sekta ya afya hivyo uwepo wa vituo hivyo utasaidia kuboresha utoaji wa huduma.
Awali akitoa taarifa ya mafanikio ya idara ya afya, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji, Dk Zaituni Hamza amesema wamefanikiwa kujenga vituo vipya saba vya kutolea huduma na kupandisha hadhi zahanati tano kuwa vituo vya afya, hivyo kufanya kuwa na jumla ya vituo vya afya 12.
Amesema kuelekea mwaka 2025, Halmashauri ya jiji inakuja na miradi ya kimkakati ikiwemo uanzishwaji wa chuo cha afya cha kati na sayansi shirikishi katika Hospitali ya Wilaya ya Kivule na kwamba jengo la kwanza tayari limekarabatiwa.
Aidha, Dk Zaituni ameishukuru Serikali kuongeza bajeti kwa Wizara ya Afya hususan upatikanaji wa dawa na vifaatiba kutoka asilimia 90.1 hadi kufikia asilimia 94 na kuahidi kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora kwa wananchi.