Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bendera za CCM, Chadema zashushwa mji wa Moshi

82621 Bendera+pic Bendera za CCM, Chadema zashushwa mji wa Moshi

Sat, 2 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Bendera za vyama vya Chadema na CCM  katika jimbo la Moshi zilizokuwa zimewekwa katika barabara na mitaa mbalimbali zimeshushwa na mgambo na maofisa wa Halmashauri  leo Ijumaa Novemba Mosi, 2019.

Uamuzi huo umeonekana kuwashtua viongozi wa vyama hivyo viwili, huku Chadema kikikitupia lawama CCM kuwa ndio kilichosuka mpango huo, wakati CCM wakiwataka Chadema kuacha propaganda.

Shughuli ya kushusha bendera hizo  imefanywa na mgambo na maofisa wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ambaye pia ni msimamizi wa Jimbo la Moshi mjini, Michael Mwandezi, amethibitisha kushushwa kwa bendera zote za vyama hivyo vyenye ushindani mkubwa kisiasa.

 

Mwandezi amesema kutokana na upandishaji holela wa bendera za vyama hivyo katika mitaa na barabara mashuhuri za mji Moshi, zimesababisha mji wa Moshi ambao ni miongoni mwa miji misafi nchini, kuonekana mchafu.

 

Mkurugenzi huyo ametaja sababu nyingine ya kuchukua uamuzi huo ni kwamba kipindi cha kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa bado hakijafika na pia Halmashauri hiyo ina sheria ndogo inayosimamia uwekaji wa mabango, vipeperushi.

 

Katibu wa CCM mkoa Kilimanjaro, Jonathan Mabhia,amekitaka Chadema kuacha kusambaza propaganda wakati ushushaji huo wa bendera pia umekiathiri CCM.

 

"Kwa sasa nisingependa kuzungumzia hili suala mpaka nitakapopata maelezo kutoka mamlaka zinazohusika. Nimeambiwa kuwa kuna watu walikuwa na gari la Serikali ndio wameshusha hizi bendera. Tunafuatilia," amesema Mabhia.

 

Mabhia aliwataka Chadema kuacha kueneza propaganda chafu kuwa CCM kinahusika na ushushwaji huo wa bendera wakati ni kazi iliyofanywa na mamlaka za Serikali.

 

Katibu wa Chadema mkoa Kilimanjaro, Basil Lema amesema kushushwa kwa bendera hizo kuna mkono wa CCM kwa madai kuwa wingi wa bendera hizo unaonyesha uhalali wa chama katika eneo husika na Moshi mjini ni ngome ya Chadema.

Chanzo: mwananchi.co.tz