Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bawacha yalaani Mauaji ya Watoto

39432 Lawapic Bawacha yalaani Mauaji ya Watoto

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) limelaani mauaji ya watoto yaliyotokea mkoani Njombe huku likiitaka Serikali kuchukua hatua za kisheria kudhibiti vitendo hivyo.

Katika waraka wa Bawacha ulioandikwa na mwenyekiti wake, Halima Mdee umetoa salamu za rambirambi kwa ndugu wa familia zilizokumbwa na msiba huo huku akisema vitendo hivyo havikubaliki katika jamii.

Mdee ambaye pia ni mbunge wa Kawe ameeleza kuwa sababu zinazotajwa kuwa mauaji hayo ni ya kishirikina hazitakiwi kuungwa mkono na badala yake, juhudi za makusudi zichukuliwe kukomesha vitendo hivyo.

Hadi sasa watoto 10 wametekwa na kuuawa kati yao, watatu ni wa familia moja katika Halmashauri ya Mji wa Njombe na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.

“Bawacha Taifa tunalaani vikali mauaji hayo na wote wanaohusika na unyama huo dhidi ya watoto ambao ni mojawapo ya makundi maalumu katika jamii yetu yanayostahili kulindwa, kupendwa na kuthaminiwa, si kufanyiwa ukatili wowote ule,” imesema taarifa hiyo.

Jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola aliliambia Bunge kuwa mauaji hayo yanasababishwa na imani za kishirikina ikiwamo kutaka utajiri na kuongezewa vyeo kazini.

“Tumeshapata orodha ya wahusika na majina ya wahusika na tumebaini sababu kubwa ni ushirikina lakini nawaonya wote wanaohusika kuwa wasitingishe kibiriti kwenye Serikali ya Rais John Magufuli watashughulikiwa,” alisema Lugola.

Bwacha wameitaka wizara hiyo kutekeleza tamko hilo kwa vitendo kwa kutumia mamlaka za kisheria kutokomeza vitendo hivyo.

“Tunasisitiza suala la kudhibiti mtandao wa wahusika, kwa sababu katika miaka ya hivi karibuni Watanzania wameshuhudia kuongezeka kwa vitendo vya utekaji, mauaji na kutelekezwa kwa miili ya watu waliouawa lakini hawaoni hatua madhubuti za kukomesha hali hiyo,” imesema.

 

Soma Zaidi: Sakata la watoto kuchinjwa Njombe ni mshikemshike



Chanzo: mwananchi.co.tz