Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bawacha walia na mikutano ya hadhara

BAWACHA Bawacha walia na mikutano ya hadhara

Thu, 8 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakati Disemba 9, 2022 ni maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru, Baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha) limetaka mikutano ya hadhara iruhusiwe ili kuvipa uhuru vyama kufanya siasa.

 Mbali na mikutano ya hadhara, pia baraza hilo limetaka Rais Samia kukamilisha mchakato wa katiba mpya na upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi kabla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

Serikali ilizuia mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa mwaka 2016, ikitaka wananchi wajikite kwenye shughuli za maendeleo hadi wakati wa chaguzi nyingine.

Hata hivyo, katazo hilo lilizua manung’uniko kutoka kwa wadau wa demokrasia ndani na nje ya nchi.

Miongoni mwa wadau hao ni Kikosi kazi cha kukusanya maoni ya demokrasia kilichokabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan Oktoba 21 mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine kimependekeza mikutano ya vyama vya siasa iruhusiwe.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Desemba 7, 2022 Katibu mwenezi wa Baraza hilo Aisha Machano amesema wanawake wamekuwa wahanga kutokana na kushindwa kufanya shughuli za kisiasa.

"Wanawake hatuwezi kufanya shughuli za kisiasa kama hakuna mikutano ya hadhara, kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru tunamshauri Rais aruhusu mikutano ya hadhara,"amesema.

“Rais aliahidi kushughulikia suala hili lakini bado, wanawake tunategemea mikutano ya hadhara ili kuweza kujijenga na kujiimarisha," amesema Machano.

Chanzo: Mwananchi