Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bashiru akerwa wasomi kuwa na uchu madaraka

47103 Pic+bashiru

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema anakerwa na baadhi ya wanataaluma wa vyuo vikuu kuwa na njaa ya madaraka, na kuwataka kuhakikisha michakato ya kuwapata viongozi inazingatia sifa, uwezo na uadilifu.

Dk Bashiru aliyasema hayo juzi usiku wakati wa hafla fupi ya kumuaga iliyoandaliwa na Umoja wa Jumuiya za Wanataaluma wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma Tanzania (Asapuct), ambayo yeye alikuwa makamu wa rais.

Hafla hiyo ya kumuaga ilifanyika baada ya Mei 29, mwaka jana, kuteuliwa kuwa katibu mkuu wa CCM kuchukua nafasi iliyoachwa na Abdulrahman Kinana.

Dk Bashiru alisema matatizo mengi yaliyomo katika sekta ya elimu nchini mengine suluhu yake siyo fedha, bali mawazo mapya, ubunifu, misimamo na mtazamo wa Watanzania.

“Kwenye elimu hakuna jambo linalonikera na nadhani linawakera watu wengi kama wanataaluma nao kuwa ni watu ambao wana njaa ya madaraka,” alisema.

Awali, Rais wa Asapuct, Dk Paul Loisulie alisema wamefanya uchambuzi wa bajeti na kushauri mambo mbalimbali ikiwamo kurudishwa kwa muda wa hati za kusafiria uliokuwa ukitolewa zamani kwa watu wanaotaka kusafiri katika nchi za Afrika Mashariki.

“Ukipewa pasipoti hii ukaenda na kurudi basi muda wake umemalizika, huwezi kuitumia tena, kwa hiyo tunawanyima Watanzania fursa ya kuwasiliana na wenzao wa Afrika Mashariki,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk Francis Michael alisema Serikali imeendelea kuwapandisha vyeo wanataaluma, ingawa katika maeneo mengine wamesimamisha.



Chanzo: mwananchi.co.tz