Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bashiru ajadiliwa kauli ya kutumia dola kubaki Ikulu

98380 Bashiru+pic Bashiru ajadiliwa kauli ya kutumia dola kubaki Ikulu

Mon, 9 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akisema vyama tawala hutumia dola kubaki madarakani na vinavyoshindwa ni kwa sababu ya uzembe, Katibu Mkuu wa Chadema amesema chama hicho kitatumia nguvu ya umma kuiondoa madarakani.

Dk Bashiru alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari vya IPP Media jijini Dar es Salaam, akisema vyama tawala vinavyoshindwa uchaguzi ni kwa uzembe kwa kuwa vina kila kitu cha kusaidia kubaki madarakani.

Lakini akaonya kuwa kinachotakiwa si kutumia dola kunyanyasa washindani wako.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua mafunzo ya Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha) Mnyika alisema: “Kama wao wanatumia dola kubaki madarakani, sisi tutatumia nguvu ya umma kuwaondoa madarakani.”

Mnyika, ambaye alikuwa akizungumzia hali ya siasa kwa miaka mitano tangu mwaka 2015, alisema kwa kauli ya Dk Bashiru ni wazi kuwa Serikali haina dhamira ya kuunda tume huru ya uchaguzi.

“Kwa ukimya wa Rais baada ya kuandikiwa barua na mwenyekiti (Freeman) Mbowe na Chadema kuhusu tume huru ya uchaguzi, inaashiria kwamba kimsingi hawana dhamira ya kuleta tume huru ya uchaguzi na wana dhamira ya kuitumia dola kubaki madarakani,” alisema Mnyika.

Pia Soma

Advertisement
Mbali na Mnyika, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wametoa maoni tofauti kuhusu kauli hiyo na mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alihoji mamlaka ya viongozi wa vyama vya siasa yakiwemo ya mwenyekiti wa chama tawala kuteua viongozi na watendaji wa tume ya chaguzi.

“Kauli hiyo lazima itakuwa imewakera wapinzani ukichukulia madai ya demokrasia waliyonayo na jinsi chama tawala kinavyochukulia. Dk Bashiru hakutoa kauli hiyo kidiplomasia,” alisema.

Alisema chama tawala kina uwezo wa kutumia vyombo vya dola kuendelea kuaminika kwa wananchi, lakini akasema kwa joto la kisiasa lililopo kwa mwaka huu, kauli hiyo ni lazima itazua maswali mengi.

“Watu wanatafsiri tofauti hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika uchaguzi mkuu. Hata hivyo, bado vyama vya upinzani vinaweza kushinda hata kama vyombo vya dola viko chini ya chama tawala kama vitaushawishi umma,” alisema.

Alisema inategemea na chama tawala, lakini vyama tawala vimekuwa vikiangushwa sehemu mbalimbali duniani.

Hata hivyo, Dk Stephen Mwakalinga, kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala, alisema kauli hiyo imeeleweka vema kwa vyama vya upinzani na wananchi kwa ujumla jinsi vyombo vya dola vinavyotumika.

“Tuwe wazi kwamba vyama vya siasa nchini na kokote duniani vinapambana kushika madaraka kwa lengo la kuwa na mamlaka ya vyombo hivyo. Kama isingekuwa faida hiyo, tusingeona kampeni kali kama hizo nyakati za uchaguzi,” alisema.

“Dk Bashiru alikuwa sahihi kabisa. CCM inayo nafasi kubwa ya kuendelea kutawala, lakini hiyo haimaanishi kuwa wanaweza kuvunja sheria. Kwangu ilikuwa ni ujumbe wa kawaida tu kama unavyoweza kusemwa na mtu mwingine wa chama hicho,” alisema.

Mchambuzi mwingine wa siasa, Thomas Ombeni alisema popote pale duniani vyama tawala havilinganishwi na vyama vya upinzani.

Alisema ni wakati wa uchaguzi mkuu, vyama vya upinzani vikivishinda vyama tawala navyo hupata mamlaka hayo.

“Tunapaswa kujua kwamba kuwa tu madarakani ni faida. Hata hivyo, vyama vyote vya upinzani vinapaswa kuwa makini kwa vinayoyasema sasa wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz