Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bashiru: Tutalihifadhi eneo la ukombozi Kongwa

4a408bcb22cdcd302b9218b302433ec8 Bashiru: Tutalihifadhi eneo la ukombozi Kongwa

Mon, 28 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Kongwa ilikuwa uwanja wa mapambano ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na kuna mikakati ya kuhifadhi eneo hilo.

Kimesema katika Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25, kuna mikakati iliyoanishwa ya kuhifadhi maeneo ya kihistoria nchini, ambayo wapigania uhuru waliishi na kupanga mikakati ya mapambano, ikiwemo eneo la Kongwa.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally Dk katika mkutano wa kuzindua awamu ya tatu ya kampeni za CCM, kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Awamu ya kwanza ya kampeni za CCM, ilizinduliwa Dodoma Agosti 29 jijini Dodoma na awamu ya pili ilizinduliwa mjini Bukoba mkoani Kagera.

“Awamu ya nne ya kampeni zetu tutaizindua Zanzibar na tunazo awamu sita. Na kila awamu ina mikakati maalumu kuliko awamu iliyotangulia,”alisema Dk Bashiru.

Dk Bashiru alitaja maeneo muhimu yanayotambulika kwa kutumika katika mapambano hayo ya ukombozi wa Afrika nchini kuwa ni Dodoma, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Pwani, Morogoro na Dar es Salaam.

“Haya ni maeneo yaliyobeba alama ya kumbukumbu ya mapambano ya ukombozi wa Afrika chini ya TANU na baadaye CCM. CCM ni chama kilichorithi kazi ya ukombozi wa Afrika,” alisema Dk Bashiru.

Alisema wagombea ubunge, udiwani na uwakilishi wanafanya takribani mikutano 600 kila siku. Alisema Mgombea Urais John Magufuli, Mgombea Mwenza Samia Suluhu Hassan na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, Kassim Majaliwa kwa ujumla wanafanya mikutano 20 kila siku kitaifa.

Alisema pia wajumbe wa Kamati Kuu, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda na Mgombea Ubunge wa Kongwa, Job Ndugai na wajumbe wote wa Kamati Kuu, wanaendelea kufanya kampeni za mikutano ya hadhara, mikutano ya ndani, mikutano ya kimkakati na makundi na kampeni za nyumba kwa nyumba na kitanda kwa kitanda.

Alisema chama hicho kimeamua kuzindua awamu za kampeni zake maeneo mbalimbali, kwa sababu Tanzania nzima ni nchi ya mashujaa. “Sisi sote ni kizazi cha mashujaa wa ukombozi wa Bara la Afrika, hatujafanya makosa kuzindua awamu ya tatu hapa Kongwa kwa sababu tupo kwenye ardhi ya mashujaa ambao hawaogopi kitu,” alisema.

Dk Bashiru alisema wapinzani wanaweza kufanya mambo matatu, ambayo ni kuhamia kwenye chama hicho na watawapokea, kustaafu siasa bila kusababisha vurugu au kuvijenga upya vyama vya kitaasisi ili vishindane na CCM.

“Kustaafu siasa ni ruksa, kwanza tunaambiwa wengine wana tiketi za kurudi Ulaya, lakini wastaafu na kuondoka taratibu na si kwa kuchonganisha taifa letu,” alisema na kuongeza; Kwa upande wake, Samia alieleza mikakati ya CCM kupitia Ilani ya chama hicho kwa mkoa wa Dodoma hususani Kongwa katika kuboresha barabara, maji, nishati, elimu, afya na ardhi kwa wananchi.

Alisema pamoja na hayo, Serikali ya Awamu ya Tano ikipatiwa ridhaa inajipanga kujenga vituo vya afya na zahanati 98, kujenga hospitali za wilaya 10 katika maeneo ambayo hayana hospitali hizo na kuimarisha mfumo mzima wa bima ya afya ili kila mtu anufaike na huduma za afya.

Aidha, alisema kupitia ilani ya chama hicho wanakusudia kuendelea kupatia ufumbuzi migogoro ya ardhi, kupitia kamati ya mawaziri pindi tu watakaporejea madarakani. Ndugai alisema kwenye mkutano huo kuwa, wapinzani kitaifa wamekosa hoja.

Chanzo: habarileo.co.tz