Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bashiru: Ruksa wabunge wa CCM kuikosoa Serikali

9799 Bashiru+pic TZWeb

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema ni ruksa kwa wabunge wao kuikosoa Serikali, lakini akatoa angalizo; wasitumie lugha kali, wasizushe wala kutia chumvi mambo wasiyo na uhakika nayo.

Alikuwa katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Dodoma.

Msomi huyo alisema mbunge atakayeitetea Serikali ya CCM ambayo imewekwa madarakani na wananchi, pia hatakuwa amefanya kosa.

“(Wabunge wa CCM) Waisimamie Serikali na waikosoe kwa ushahidi na kwa hoja, ama hadharani katika Bunge,” alisema Dk Bashiru.

“Lakini kwa kufuata taratibu za kibunge au ndani ya kamati ya wabunge wa CCM.”

Alisema hiyo ni kwa sababu kamati ya wabunge ina uongozi na taratibu zake na kwamba katika kamati hiyo wabunge hukosoana waziwazi na kuambiana ukweli kuliko hata wanavyofanya hadharani.

“Kwa sababu mbunge wa CCM ana chama chake, ana wapigakura wake, ana haiba yake mwenyewe na msimamo wake na ana Taifa lake, maeneo haya manne anahitaji kuyawekea uwiano,” alisema mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Maeneo haya yana masharti. Huwezi ukawa mbunge unaisifu Serikali inayoelekeza mambo ambayo yanaharibu uchumi, huo sio utaifa. Ndio maana hata mwalimu alifikia mahali akasema ‘CCM sio mama yangu. Kama CCM inaweza kuwa na mambo ya ovyo naweza kuachana nayo’.”

Alisema ndio maana kuna wakati Mwalimu Nyerere alimuunga mkono mgombea wa upinzani.

Alisema alifanya hivyo kwa sababu alidhani mgombea aliyeteuliwa na CCM hakuwa anafaa na yule aliyeteuliwa na upinzani alikuwa anafaa.

“Kwa hiyo mwalimu hapo alikuwa hasaliti chama chake, alikuwa anasimamia nchi. Huwezi kukubali mtu wa ovyo ashinde kwa sababu ni CCM. Kazi yetu ndani ya chama ni kuhakikisha tunachuja wagombea wetu ili wale tunaowatoa wawe wanakubalika,” alisema.

“Na (wabunge wa CCM) wakishashinda, wanakwenda kujiwakilisha wao wenyewe kwa nafsi zao kama Watanzania, kukiwakilisha chama, wapigakura ambao ni wana CCM na wasio wanaCCM na nchi yao,” alisema Dk Bashiru.

Hata hivyo, Bashiru alisema kwa bahati mbaya wabunge wa pande zote mbili wameshindwa kuweka uwiano wa maeneo hayo.

“Wengine ukiwasikiliza ni porojo zao. Wamedandia hoja fulani lakini wengine ukiwasikiliza wameegemea kwenye chama zaidi. Lakini msimamo ule una madhara kwa wapiga kura wake ambao wengine si wanachama wa chama chochote,” alisema.

Alisema ukisikiliza wabunge wengine, unaona hawana mtazamo wa kitaifa na wanakuwa wanavuta sehemu moja.

“Kwa hiyo ni kazi ya kuelimishana na tunafanya hivyo kwenye vikao na kwenye kamati kuhakikisha kuwa wabunge wanatoa michango yao kwa nguvu zao zote, vipaji vyao vyote, kusimamia maslahi ya nchi yao, maslahi ya chama wapiga kura wao na taifa,” alisema.

Dk Bashiru alisema wakipatikana wabunge wa aina hiyo, wanaoangalia maslahi ya kila upande bila kujali wanatoka kambi gani, Tanzania itakuwa na Bunge imara la kuisimamia Serikali.

Demokrasia ya uwakilishi

Kuhusu kuingiliwa uhuru kwa wabunge wa CCM wanapochangia mijadala, Dk Bashiru alisema wamekubaliana na uongozi wao na wanafanya mpango katika Baraza la Wawakilishi kuhakikisha kuwa sekretarieti ya chama inafuatilia mwenendo wa utendaji wa wabunge wa chama hicho katika vikao vya maamuzi.

Alisema mbunge anayelalamika kuminywa kwa uhuru wake akihisi kamati ya uongozi wa chama hicho imemnyima uhuru wa kuzungumza katika chombo cha maamuzi, aende kumueleza.

“Juzijuzi nimezungumza naye vizuri (mmoja wa wabunge wa CCM) na tutakuja kukutana naye. Ni kijana ambaye ana mawazo ya kujenga na ana misimamo lakini tukubaliane kuwa si kila unachokiamini lazima kikubalike katika mjadala,” alisema Bashiru na kuongeza.

“Kama mtu mvumilivu lazima ifike mahali ujue kuwa mawazo yatakayotawala maamuzi, ama yanaweza kuwa sehemu ya mawazo yako au yakatofautiana na mawazo yako. Kwa hiyo sitarajii kabisa vyombo hivi vikawa na mawazo yanayofanana.”

Alisema iwapo kuna taratibu ambazo zinawanyima nafasi ya kuzungumza wabunge wa CCM, utaratibu huo hautaruhusiwa.

“Tunahitaji kamati za wabunge ziwe imara ziwe na mazingira huru ya kukijenga chama ndani ya Bunge sio kuwaingilia wabunge uhuru wao, lakini ukishakuwa mwanachama ukubali umeugawa uhuru wako,” alisema.

“Ni suala la kugawagawa tu. Ni sawa na ndoa, unagawa kidogokidogo. Kama nilivyosema ni makundi manne hapo. Ni kweli uhuru wa wabunge umegawanyika na hakuna Bunge duniani ambako utakuta ubunge wao uko kamili na ukikuta hivyo, hilo halitakuwa Bunge bali ni kundi fulani,” alisema.

Alisema Bunge ni lazima litakuwa na utaratibu ambao unamnyang’anya uhuru mbunge lakini uhuru huo lazima uwe na maslahi kwa Taifa au kwa wapigakura, mbunge mwenyewe au chama.

“Labda kama (mbunge) anasema chama kimechukua kipande kikubwa kuliko vingine, hilo linajadilika. Mimi ningetaka chama kiweke utaratibu wa kuwapa uhuru wabunge kutumia vyombo hivyo kama kamati za Bunge na kamati ya wabunge wa CCM kuwa vyombo vya majadiliano na mashauriano,” alisema.

Hata hivyo, alisema majadiliano yawe ni ya kukosoana lakini wasitumie lugha kali, wasizushe mambo, wasiweke chumvi kwa jambo ambalo si la kweli na waibue mambo mapya ya maslahi ya wananchi.

Vyombo vingine

Dk Bashiru pia alisema si kila kitu kinachozungumzwa kina maslahi na wananchi na kwamba Afrika haijafikia kiwango cha Bunge linazungumza masuala ya wananchi wakati wote.

“Sauti ya wananchi haiwezi kusikika kwenye Bunge la kitaifa tu,” alisema.

“Tungeimarisha vyombo vya vijiji na kuheshimu maamuzi ya vyombo vya serikali za kijiji na wilaya, matatizo mengi yangesemwa na kutatuliwa na vyombo hivyo. Wabunge wasisahau tunapoimarisha nguvu ya Bunge lazima tuimarishe vyombo vingine vya maamuzi vya chini.”

Alisema demokrasia ya kweli katika nchi masikini kama ya Tanzania ni kuwa vyombo imara vya maamuzi vya chini ambako ni karibu na wananchi.

“Nenda kule vijijini ni mikutano mingapi ya vijiji inafanyika? Hakuna anayeratibu na anayejali lakini ipo kikatiba. Akishachaguliwa, anasubiri uchaguzi mwingine hakuna anayejali. Tunataka wabunge wetu wasibebe demokrasia ya kibunge pekee kama ndio demokrasia pekee.”

Pia alisema demokrasia katika ngazi ya vijiji inatakiwa ipate nguvu kwa kuwa ndiko matatizo makubwa.

“Nani anaratibu maoni kwenye mikutano inayofanyika chini ya miti vijijimi na ni nani anasikiliza?” alihoji.

Alisema CCM inataka kuona vyombo vyote vya maamuzi vinapata nguvu na sauti zake zisikilizwe, lakini bahati mbaya Bunge ndilo linaonekana ndio chombo pekee cha uwakilishi.

Alisema asilimia 70 ya serikali za vijiji na asilimia 65 za serikali za mitaa na halmashauri zipo chini ya CCM na ndivyo atakavyoshughulika nazo.

Chanzo: mwananchi.co.tz