Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bashiru: Nimekuwa mwana CCM tangu mwaka 1994

10119 Pic+bashiru TZW

Thu, 28 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally anatimiza mwezi mmoja kwenye wadhifa huo baada ya kubeba mikoba ya Abdulrahman Kinana. Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, msomi huyo wa siasa pamoja na mambo mengine anaeleza jinsi atakavyorejesha misingi ya Azimio la Arusha anayosema iliporomoka muda mrefu.

Swali: Hongera kwa kuteuliwa kuwa katibu mkuu wa CCM. Ulijisikiaje ulipopewa taarifa ya wadhifa huu?

Jibu: Ni wadhifa mkubwa kwa maana ya majukumu ya nafasi yenyewe, kwa maana ya taasisi iliyoniteua (CCM) na nilifurahi kwa kuona kuwa nimeheshimiwa na kutambuliwa mchango wangu. Nikajenga matumaini kwamba imani niliyopewa ni dhamana ambao ni lazima niitumikie kwa utii ili walioniteua wakidhi matarajio yao.

Swali: Je, ulipata fununu zozote kwamba ungepewa cheo hicho au walikushtukiza tu?

Jibu: Unajua suala la uteuzi katika CCM liko bayana katika katiba yake, si suala la fununu. Mimi sikupata fununu yoyote, bila shaka kuna utaratibu uliofuatwa na katika kikao kile jina langu likatangazwa ndiyo nikajua kwamba mwenyekiti ameshapendekeza jina langu. Nikaona shamrashamra kwa wajumbe na mimi sikufanya ajizi nikakubali.

Ingawa magazeti yalishaanza kuandika, na siyo wakati huu tu, nadhani tangu mwaka 2016 hata mitandao. Hata kabla katibu mkuu mstaafu hajaondoka. Kwa hiyo, kama ni suala la fununu, zilikuwa kwenye magazeti hata kabla sijafanya kazi kwenye tume ya mali za chama.

Swali: Umekuwa mwanachama wa CCM tangu lini?

Jibu: Kuwa mwanataaluma ni sehemu ya kuwa mwana siasa. Kuwa mwanahabari ni sehemu ya kuwa mwanasiasa. Kwa hiyo ukishafanya kazi inayohusu maisha ya watu, ukishafanya kazi kwenye jamii umeshakuwa na mchango, ukiwa na mahitaji kama binadamu katika jamii, unaweza kuwa mwanasiasa, lakini kuwa mwanachama ni jambo la hiari.

Ndani ya CCM ili kuwa mwanachama ni lazima uombe kwenye tawi lako; na mimi nimekuwa mwanachama si wale wa kurushiwa kadi wakati wa uchaguzi, au kukatiwa kadi na mgombea ili nimchague.

Kwa hiyo tangu enzi za mfumo wa chama kimoja, ukishasoma kwenye shule ya umma na ukapata uongozi katika shule ile, ilikuwa ni sharti uwe kiongozi wa umoja wa vijana wa CCM. Kwa hiyo hakukuwa na hiyari.

Kwa hiyo mimi ni mwanachama tangu mwaka 1994 katika kijiji changu cha Kanazi na kadi yangu ninayo, na ina namba za usajili, na ukitaka kwenda Kanazi utapata taarifa zangu. Ukitaka ushahidi ninaweza kukupa hata namba za katibu wangu.

Nilipokwenda chuo kikuu mwaka 1997 nilikuta pale hakuna tawi la chama, siasa zilikuwa haziruhusiwi kama wakati wa mfumo wa chama kimoja. Kwa hiyo mimi nilishakuwa mwanachama, nilishakuwa katibu mwenezi wa CCM kwa uchaguzi wa mwaka 1997 katika Kata ya Katerero na mwaka huo nikagombea kuwa mwenzi wa wilaya ya Bukoba Vijijini nikashindwa.

Mwaka 1997/98 nikaja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nikaja na kadi yangu. Tunaanza mchakato wa kujenga tawi la Abiani. Nikachangia pesa ya posho ya chuo, wakati huo tunapewa mikopo.

Kwa hiyo nimeshiriki kwenye shughuli za chama enzi za chama kimoja na wakati wa vyama vingi, tena nikiwa kiongozi.

Kwa hiyo kuna watu wanadhani nilipewa kadi siku hiyohiyo ya uteuzi, wengine wakasema ameionyesha kadi ili watu waamini, lakini nilikuwa natania, kwa sababu huwezi ukapewa uanachama kwa kupewa kadi siku hiyohiyo. Ulikuwa ni utani tu na mimi nilikuwa nawajibu watani zangu tu.

Swali: Ukiwa mhadhiri ulikuwa ukiikosoa Serikali na CCM, hivi hukuwahi kufikiria kwamba siku moja unaweza kuwa mtumishi wake?

Jibu: Hii nafasi siyo ya kugombea, huwezi kujaza fomu ukapata wadhamini, wakakufikiria wakakupitisha. Kikatiba kazi hii ni ya uteuzi, na taratibu zipo, unafikiriwa halafu unapewa kazi. Kwa hiyo nisingeweza kufikiria kama ningeweza kuifanya.

Pia, nilikuwa katika taaluma, Kwa hiyo fikra zangu zilikuwa ni za kitaaluma. Kwa hiyo unaweza kuandika makala, ukaziwasilisha, zikahaririwa, zitatathminiwa halafu ukapata cheo cha kitaaluma.

Kwa hiyo mimi tangu nilipoajiriwa na Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2003 na mwaka 2004 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kweli matarajio yangu yalikuwa ni vyeo vya kitaaluma na nimevipata mpaka nilipoingia kwenye utumishi wa chama. Kwa hiyo si jambo ambalo nilitegemea kwa sababu halikuwa kwenye mpangilio wa maisha yangu ya kitaaluma.

Lakini, halikunishangaza kwa sababu nimekwambia tangu mwaka 1994 nimekuwa mwanachama na nimetoa mchango ambao mwingine siyo wa dhahiri. Ushauri, utafiti, uchambuzi na hayo yote sioni kama nimependelewa au nimechomolewa na kupachikwa.

Swali: Ulipoingia kwenye ukatibu mkuu, umekikuta chama katika hali gani?

Jibu: Kwanza nimekikuta chama kiko katika hali ya kuleta mabadiliko ndani na katika Serikali. Kwa upande wa chama katiba ya sasa ya mwaka 1977 imebadilisha mambo kadhaa. Moja ya mambo hayo ni kupunguza idadi ya wajumbe kwenye vikao.

Ni utaratibu ambao huwezi kuwa na vyeo viwili kwa wakati mmoja. Ndiyo maana ukiangalia kwenye halmashauri kuu idadi imepungua, lengo ni kuwa vikao vya kazi siyo kama mkutano wa hadhara, upande mwingine mnaongeza ufanisi.

Nimekuta utaratibu mpya wa kuchagua wagombea. Kwa sasa utaratibu ni kwamba hawatakuwa wanachama wote, bali vitakuwa vyombo vya kikatiba vitakavyoendesha ushindani ndani ya chama na huu ni utaratibu mpya kabisa.

Lengo ni kuhakikisha uchaguzi ndani ya chama unasimamiwa kwa haki na utaratibu wa kuwapata watendaji hauyumbishi chama.

Kwa upande wa usimamizi wa mali, katiba yetu ya sasa inasema mali zote za jumuiya yaani Umoja wa Vijana, Wanawake na Wazazi zitakuwa chini ya Baraza moja la wadhamini. Huko nyuma kila jumuiya ilikuwa na baraza lake.

Lengo ni kuhakikisha kwamba rasilimali za chama zinasimamiwa vizuri, kwa umadhabuti na kwa uwazi. Hili ndilo nimelikuta kubwa na ndiyo sababu ya Tume niliyoiongoza ya kuhakiki mali za chama.

Swali: Tume ile ilikuwa na kazi gani hasa?

Jibu: Tume ile ililenga kuhakikisha mali zote za chama zinatambuliwa, ziko wapi, kiasi chake na zina hali gani, zinasimamiwaje, zipi sio salama, zipi zimeibiwa na ni utaratibu gani tutafanya zile mali ziweze kuwa na mchango katika kuwezesha chama kujitegemea kiuchumi.

Swali: Kwa hiyo hali mmeikutaje?

Jibu: Unajua wewe ni Mtanzania, unajua hali yetu ya usimamizi ilivyo na unajua mambo yanavyoendelea hata kwenye serikali, kwa hiyo kama unaona matatizo ya usimamizi ya mali ndani ya Serikali, ukiwa mkweli ndivyo mambo yalivyo hata kwenye chama.

Kwa ujumla kuna tatizo katika nchi yetu la kutosimamia mali zetu na tatizo la kutowajibika kwa wale waliopewa dhamana ya kusimamia mali hizo. Tatizo la kutokuwa na maarifa ya kutosha ya kusimamia rasilimali hizo.

Haya mambo yako kwenye vyama vyote, taasisi zote za kiserikali, sekta binafsi, yapo kwenye asasi zisizo za kiserikali.

Kwanza kiwago cha maarifa ya usimamizi wa mali za chama kiko chini na mapendekezo yaliyofanywa ni lazima tuongeze maarifa, kama tunataka kupata ushauri kiuchumi, kifedha tufanye hivyo.

Tatizo la pili, kulikuwa kuna aina fulani ya udokozi wa mali, wakati mwingine taratibu za kusimamia mali hazikufuatwa, wakati mwingine mali zina thamani kubwa lakini mchango wake ni mdogo, wakati mwingine mikataba ya watu ambao tumeingia nao tushirikiane ili kuwa na matatizo.

Maeneo yote hayo tumependekeza na wameanza kushughulikiwa. Matarajio yangu ni kwamba zile hatua zitasimamiwa na bahati nzuri nimepewa jukumu hilo kusimamia mapendekezo yale.

Swali: Watu waliotajwa katika ripoti hiyo mtawachukulia hatua gani?

Jibu: Hilo si swali gumu kulijibu, kwa sababu unaona katika serikali dhana ya uwajibikaji imepewa msisitizo mkubwa, ndani ya chama hatuwezi kuwa nyuma ya Serikali. Siyo kuhusu ripoti hii tu bali kuhusu mambo yote. Mtu akipewa jambo asipotekeleza utaratibu wa kumwajibisha upo.

Kwa hiyo sina shaka, wale wote ambao walipaswa kuwajibika na hawakuwajibika, utaratibu upo watawajika.

Kwa sababu tuna mahitaji makubwa ya fedha ndani ya chama. Tuna watumishi wengi wanahitaji kulipwa, tuna watu kama 1,000 wanahitaji kulipwa kila mwezi, tuna vitendea kazi kama magari, majengo yanayoitaji kuhifadhiwa na kusimamiwa na yote yanahitaji maarifa na mbinu.

Swali: Umekuwa muumini mzuri wa Azimio la Arusha hasa katika mijadala mbalimbali. Unadhani bado linatekelezwa na CCM?

Jibu: Swali zuri nilitamani hili ndilo lingekuwa la kwanza. Azimio la Arusha ni waraka wa kihistoria na ni waraka wa kimapinduzi na umeitwa hivyo si na sisi Watanzania tu bali hata wachambuzi wengine kwa sababu ya falsafa zake. Kwa hiyo ni zaidi ya kuwa waraka wa Tanu na baadaye wa CCM, kwa kweli ni waraka wa kifalsafa, kinadharia na kisiasa.

Waraka huu unahusu mwana CCM na asiye mwana CCM. Haukuandikwa ili kuongoza itikadi za CCM bali uliandikwa kwa ajili ya kuendesha siasa nchi katika sera ya ujamaa na kujitegemea.

Kwa hiyo mimi kwa maoni yangu, huu ni waraka ambao haujatekelezwa ipasavyo, siyo kwa CCM tu bali kwa Watanzania wote. Nitakuwa mnafiki kusema kuwa CCM imefanya juhudi za kutosa kuutafsiri ule waraka, kuuchambua na uufanyia kazi kulingana na wakati uliopo.

Swali:Unasema azimio limeporomoka, mnachukua hatua gani kama chama?

Jibu: Katika kipindi hiki cha awamu ya tano na chini ya uongozi wangu. Juhudi kubwa tutaziwekeza kufanya kazi hiyo. Kuuchambua ule waraka, kuutafsiri, kuulinganisha na hali halisi tuliyonayo, ili uweze kuwa mwonozo hhalisi aika chama chetu, hasa katika maeneo matatu.

Eneo la kwanza ni maadili ya uongozi. Mle katika zmio la Arusha kuna masharti yaliyokuwa yanataka kumwekea kibano kiongozi mwenye madaraka kutimiza wajibu wake bila kujinufaisha. Masharti yale yalipoyumba ndiyo unasikia lugha za ufisadi na kutumbua majipu.

Wakati wa Azimio la Arusha hakukuwepo ufisadi bali kulikuwa na rushwa. Rushwa ni hali ya udokozi, kujaribu kubadilisha sheria ili kumnufaisha yule. Hiyo ipo. Lakini ufisadi wa kuchukua ardhi kwa madaraka yako na usiitumie ukakaa unaaiangalia tu bila kuwaangalia wenzako.

Ufisadi wa kuiba fedha benki kuu, ukaanza kuvaa suti na kukaa kwenye hoteli za kigeni, ufisadi wa kuibiwa nchi na kuipunguzia uwezo wa kujiendesha. Hilo ni eneo moj tutalizingatia.

Tumeanza, na bado kuna wasiwasi. Sasa hivi huwezi ukaiba fedha za Taifa halafu ukatamba barabarani, huwezi. Huo ndiyo ukweli. Ndani ya chama tutaendelea kuihimiza Serikali wasitumie vibaya dhamana zao.

Eneo la pili ni njia ya maendeleo. Ili tuendelee tunatakiwa tufanye kitu gani. Azimio la Arusha liliweka bayana kwamba huwezi ukaiondoa dola katika shughuli za uzalishaji na uongozi wa uzalishaji katika sekta ya uchumi. Sisi katika hiyo kanuni tumelegalega.

Tukaifunga dola mikono, macho ya dola tukayaondoa, pua tukaziziba, halafu tukasema jukumu la maendeleo ya nchi hii ni Ia sekta binafsi. Sekta binafsi iko wapi? Ni wawekezaji wa nje. Kilichotokea ni kwamba, benki hatuna udhibiti nazo. Hata benki tuliyokuwa nayo, tukaiuza kwa bei chee, mashirika ya umma tukayasimamia vibaya na mengine tukayafisidi, madini tukayasimamia vibaya na ardhi tukaachia.

Sasa hivi tunataka kurudisha nchi katika mstari wa maendeleo. Kwa maana kwamba dola lazima iweke malengo na masharti yanayowezesha kuzalisha uchumi kitaifa. Nchi zilizoendelea kama China na Vietnam zilifanya hao wanayofanya kwa kuweka misimamo yao.

Jambo la tatu ni chombo cha kisiasa kuunganisha umma na kutetea wanyonge na kusimamia hiyo siasa ya ujamaa na kujitegemea. Hicho chombo pia kililegalega. Wakati wa kufuata Azimio la Arusha, kusingekuwa na mafisadi wanaogombea na kugawa fedha hadharani ndani ya CCM. Tulifika mahali kwa sababu tulitetereka, watu wangeweza kukaa mezani na kupiga hesabu, uchaguzi wa mwaka huu una bei gani na wapiga kura wangapi tutawanunua ili tushinde na mambo hayo yalifanyika ndani ya CCM.

WASIFU

Chanzo: mwananchi.co.tz