Liwale. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewataka wanasiasa kuachana na maneno kuwa chama hicho tawala kinawanunua madiwani na wabunge wa vyama vya upinzani ili kuviua.
Dk Bashiru ametoa kauli hiyo leo Septemba 25, 2018 katika uzinduzi wa kampeni za ubunge wa Liwale na udiwani wa Kibutuka wilayani humo mkoani Lindi.
Amesema yeye ni katibu mkuu wa CCM na ndio msimamizi mkuu wa mali za chama, hivyo hawezi kuidhinisha fedha kwa ajili ya kuwanunua wapinzani kwa maelezo kuwa mikono yake iko safi.
“Habari kuwa tunanunua wapinzani si kweli. Siwezi kutoa fedha za chama kufanya hivyo. Wanaotoa kauli hizo wanakikashifu chama na mimi binafsi. Wakome,” amesema.
Amebainisha kuwa CCM ni chama makini si legelege kama vyama vingine vinavyokufa kutokana na viongozi wake wa juu kuwagawanya wanachama, sambamba na kuendeshwa kwa makundi.
Amesema chama tawala kinaendelea kutamba kwa sababu Watanzania hawapo tayari kuvikumbatia vyama vya upinzani vinavyoendeshwa kama kampuni ya mtu binafsi.
“Watanzania wanahitaji vyama vinavyoengeshwa kitaasisi na vyenye muundo, falsafa, itikadi na sera nzuri ya kuwaletea maendeleo. Vyama hivyo havipo nchini zaidi ya CCM,” amesema.