Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baraza vyama vya siasa: Sheria hizi ziboreshwe haraka

Vyama Vya Siasa Ruzuku Baraza vyama vya siasa: Sheria hizi ziboreshwe haraka

Fri, 18 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baraza la vyama vya siasa nchini limeitaka Serikali kufanyia maboresho Sheria ya Vyama vya Siasa na ile ya Uchaguzi haraka kwa lengo la kumaliza changamoto zinazojitokeza kila mara katika kukuza demokrasia ya vyama vingi nchini.

Limesema pia linaandaa kikao kitakachowashirikisha viongozi wa vyama vya siasa, dini, asasi za kiraia na viongozi mashuhuri kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo hali ya siasa nchini.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa baraza hilo, Juma Ali Khatibu alipokuwa akisoma mapendekezo ya kikao maalumu cha baraza la vyama vya siasa kilichofanyika Agosti Mosi, mwaka huu.

Khatibu alisema pendekezo jingine ni la kuwataka viongozi wa siasa kujiepusha kutumia lugha za matusi, kibaguzi, udhalilishaji, upotoshaji na kubeza wanapotaka kutimiza malengo yao ya kisiasa.

"Badala yake, viongozi wa vyama vya siasa wajikite katika kunadi sera zao kwa kujenga hoja na kutumia lugha yenye staha,” alisema Khatibu.

Alisema katika kikao hicho walipendekeza pia vyama vya siasa viepuke kuanzisha vikundi vya ulinzi vyenye mavazi na matendo yanayofanana na kutumiwa na majeshi kwa kuwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kuhatarisha amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Pia lilipendekeza taasisi za dini kujikita katika kutekeleza majukumu yao kadiri ya sheria za nchi na kujiepusha kutumia majukwaa ya kisiasa au nyumba za ibada kunadi sera za vyama vya siasa.

Alisema wamependekeza mamlaka za Serikali, ikiwemo ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, msajili wa asasi za kiraia, tume ya uchaguzi na Jeshi la Polisi ziendelee kusimamia sheria.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuweka mazingira ya amani, utulivu na umoja wa kitaifa. Wakati huo huo, Khatibu alisema baraza litafanya kikao cha kujadili mapendekezo ya kikosi kazi kilichoundwa na Rais, Samia Suluhu Hassan pamoja na hali ya siasa nchini.

Alisema kikao hicho cha siku tatu kitafanyika kuanzia Agosti 28 hadi 30 mwaka huu jijini Dar es Salaam na kitawashirikisha wadau wote wa siasa, viongozi wa dini, asasi za kiraia na viongozi mashuhuri.

Alipoulizwa kwa nini wanataka kukiitisha kikao hicho sasa, alisema ni kwa mujibu wa mpango kazi wa baraza hilo.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AAFP), Rashid Rai alisema suala la kupeleka bungeni mkataba wa bandari linaashiria nchi kupiga hatua kwenye masuala ya kidemokrasia.

Alisema mjadala uliojitokeza kuhusu bandari unaashiria kukua kwa demokrasia nchini na hiyo ni namna Serikali inavyoweza kuishirikisha jamii.

Rai alisema chama chao hakioni sababu ya kuufanya mjadala huo kuwa ni changamoto, bali ni afya kwa wananchi na wale wanaoujadili kwa faida ya nchi yao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live