Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baraza laonya vyama shinikizo Katiba Mpya

Eeb7cc1ffa28b63f92c7995e98af3cd2.jpeg Baraza laonya vyama shinikizo Katiba Mpya

Sun, 8 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VYAMA vya siasa nchini vimetakiwa kuacha kutoa mashinikizo kwa Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo madai ya Katiba mpya na kutishia kufanya maandamano nchi nzima, kwani hivyo sio vipaumbele vya msingi vya serikali vinavyotokana na matakwa ya wapiga kura.

Akizungumza na waandishi wa habari Zanzibar jana, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Juma Ali Khatib alisema huu ni wakati wa vyama vya siasa kutoa ushirikiano kwa Rais Samia ili kuimarisha uchumi na kuwaunganisha wananchi wa Tanzania kulingana na ahadi alizozitoa kwa wapiga kura badala ya kuwa chanzo cha mivutano.

Alisema wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kudai Katiba mpya na kutishia kufanya maandamano nchi nzima haina nafasi kwa sasa, kwa sababu tayari Rais Samia ameonesha utayari wa kushirikina na kufanya kazi na makundi mbalimbali nchini ikiwamo wanasiasa wa upinzani.

Alisema Rais Samia tangu aliposhika nafasi ya Urais takribani miezi mitano iliyopita, amekuwa akifanya kazi vizuri kwa kuwashirikisha wananchi na ametoa ahadi za kuyaunganisha makundi mbalimbali katika siasa na ujenzi wa taifa.

Alisema kauli za Rais Samia kuwaunganisha wananchi kupitia makundi mbalimbali zimejenga matumaini makubwa kwa wananchi wa Tanzania wenye rika tofauti kuanzia wasomi, wanasiasa na wafanyabiashara wadogo.

Khatibu alisema tabia inayofanywa na viongozi Chadema kumshinikiza Rais Samia kufanya wanachokitaka wao ikiwamo kumshinikiza mabadiliko ya haraka ya Katiba si jambo zuri kwani kila jambo linafanyika kwa wakati wake.

“Nazungumza nikiwa Mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Vyama vya Siasa nchini, huu sio wakati muafaka wa kutoa shinikizo kwa Rais Samia kufanya mabadiliko ya Katiba kwani kwa nyakati tofauti ametoa ahadi za kushirikisha makundi mbalimbali ikiwamo vyama vya siasa katika uongozi wa nchi na matokeo yake tumeyaona kwa baadhi ya uteuzi za viongozi alizofanya,” alisema.

Khatib ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Ada Tadea na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Kuteuliwa na Rais, alitoa mfano uteuzi wa aliyekuwa mgombea wa urais kupitia chama cha upinzani cha ADC, Queen Sendiga kuwa mkuu wa mkoa wa Iringa kuwa ni sehemu ya ahadi zake kuhusiana na ushirikiano na watu wote.

Alisema Rais Samia ameingia madarakani hivi karibuni na ana majukumu makubwa ya kutekeleza na kusimamia miradi ya kimkakati ambayo inalenga zaidi kuinua uchumi na kuhakikishia Tanzania inapiga hatua kubwa ya maendeleo na kuwa miongoni mwa nchi

zinazoendelea.

Khatibu alisema mafanikio hayo hayawezi kufikiwa kama Watanzania watajiingiza katika mizozano na harakati za kufanya mikutano ya kisiasa usiku na mchana pamoja na maandamano ya kudai mabadiliko ya Katiba.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir ameunga mkono kumpa nafasi Rais Samia kuendelea na majukumu yake ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama chake pamoja na ahadi zake kwa wapiga kura.

Alisema Rais Samia anaendelea vizuri tangu alipokula kiapo kuwa Rais wa Tanzania, huku akiendelea na utekelezaji wa majukumu ya msingi yanayotokana na Ilani ya chama chake, pamoja na ahadi walizotoa kwa wananchi kwa kufungua miradi mbalimbali.

“Sisi vyama vya siasa tumefarajika na kupata matumaini makubwa kwa Rais Samia tangu alipokula kiapo cha kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hata uteuzi wake wa viongozi mbalimbali unakwenda vizuri ukionesha uwiano wa watumishi wa pande mbili za Muungano,” alisema Ameir.

Msimamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kipindi cha miaka mitano ni kuendeleza, kutekeleza na kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati ambayo imo katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya 2020-2025.

Chanzo: www.habarileo.co.tz