Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baraza lakoleza mjadala wa viongozi wa dini, wanasiasa

Mutungi Pic Data Baraza lakoleza mjadala wa viongozi wa dini, wanasiasa

Thu, 3 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Viongozi wa dini nchini wameelezwa kuwa si sahihi kufanya siasa kupitia majukwaa ya vyama vya siasa, sawa na ambavyo wanasiasa nao wanatakiwa kutotumia mimbari za dini kufanya siasa.

Msisitizo huo umetokana na kile kilichoelezwa na wadau mbalimbali wa siasa na dini kuwa, hayo yote mbali na kuchochea vurugu, pia ni kinyume na utaratibu wa sheria za nchi.

Hayo yameelezwa ikiwa ni siku 12 tangu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiandikiwe barua kikidaiwa kuwaalika viongozi wa dini katika mkutano wake wa hadhara.

Barua hiyo iliyoandikwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza ililenga kukisihi chama hicho kisitishe mkutano huo, kadhalika viongozi wake walitakiwa kwenda katika ofisi yake siku inayofuata.

Chadema ilifanya mkutano huo, Juni 23, mwaka huu ukiwa maalumu kupinga mkataba wa uwekezaji na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kupitia kampuni ya DP World.

Mbali na hilo, mimbari za viongozi wa dini pia zimekuwa zikitumiwa na wanasiasa ama kutangaza masuala yenye masilahi yao ya kisiasa na vyama vyao au kuhamasisha umma juu ya jambo fulani.

Vilevile, wapo wanasiasa, wakiwemo wabunge wa kuchaguliwa ambao wanamiliki au kuongoza makanisa.

Pamoja na suala hilo ambalo limegeuka mjadala katika jamii, lingine lililojadiliwa katika kikao hicho ni matumizi ya lugha za kuudhi dhidi ya viongozi kwenye majukwaa ya kisiasa na mavazi yenye sura ya kijeshi kwa walinzi wa viongozi wa siasa.

Akizungumza katika baraza hilo jijini Dar es Salaam jana, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Alexander Makulilo alisema ingawa kuna uhusiano kati ya dini na siasa, si ruhusa kiongozi wa dini kushiriki siasa za vyama.

"Uhusiano kati ya dini na siasa ni changamani, lakini katika nchi yetu imewekwa sheria ili kuratibu uhusiano huo," alisema. Sheria hizo, alisema zinalenga kuweka mazingira mazuri ya kuleta amani, umoja na mshikamano.

Alihitimisha kwa kufafanua, "kwa mantiki hiyo sheria zinakataza chama cha siasa kutumia viongozi wa dini kufikia malengo yake ya kisiasa."

Si viongozi wa dini pekee, Profesa Makulilo alisema hata watumishi wa umma na vyombo vya ulinzi na usalama, hawaruhusiwi kushiriki siasa za vyama.

Msomi huyo alisema sheria inakataza vyama vya siasa kuwa na vikundi vyovyote vya ulinzi na usalama au mavazi yanayoashiria kijeshi, badala yake Jeshi la Polisi ndilo lililopewa kazi hiyo.

Licha ya sheria kukataza, imeshuhudiwa mara kadhaa vijana wa vyama mbalimbali vya siasa wakisimama nyuma ya viongozi wa kitaifa wa vyama hivyo, kuimarisha ulinzi, jukumu linalotajwa na sheria kuwa la Jeshi la Polisi.

Kuhusu lugha za kuudhi, profesa huyo alisema: "Hii ni kwa sababu sheria inakataza lugha za matusi, kudhalilisha, kutweza utu na kubeza kazi iliyofanywa badala yake inataka kujenga hoja mbadala, ndivyo siasa zilivyo," alisema.

Alisema sababu ya kuzuiwa kwake ni kwa sababu kuna hatari ya kutokea malumbano baina ya pande mbili.

"Leo ukimtusi kiongozi wa chama fulani kwa kuwa anakubalika na ana wafuasi, wafuasi hao nao watataka kulipa kisasi, nao watakutukana, mwisho wa hili ni hatari," alieleza.

Alipoulizwa ni sheria gani inakataza masuala hayo, Nyahoza alisema ni kifungu cha 9 (2) a) cha Sheria ya Vyama vya Siasa. Kifungu hicho kinasema “Chama cha siasa hakitastahili kusajiliwa kama kinahamasisha au kina maslahi na kundi lolote la imani ya kidini.”

Mapema akifungua baraza hilo, Jaji Francis Mutungi, msajili wa vyama vya siasa, alisema dhamira ya mkutano huo si kumnyooshea kidole yeyote aliyekosea, bali ni kuelimishana.

"Nimelazimika kusema haya kwa sababu watu huko nje wanasubiri kwa hamu kwamba hili Baraza litaisha kweli? Si watatumbuana macho?" alisema.

Matamanio yake, ni kwamba kilichoazimiwa kitatekelezwa na kila mdau wa siasa kwa masilahi ya siasa safi nchini.

Michango ya wajumbe

Akizungumza kwenye kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Joseph Selasini alieleza haja ya wanasiasa kurejea misingi ya nchi ili kuepuka migogoro.

"Sisi Wakatoliki kawaida viongozi wetu wakizungumza basi, ndiyo imeisha hiyo, sasa huyu akipanda jukwaani kusema kitu tunachukulia kama maelekezo," alisema.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Kichungaji Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Florence Rutaiwa alisema ni jukumu la viongozi wa dini kukemea dhambi inayofanywa na binadamu.

“Lakini kiongozi huyo hapaswi kutumia jukwaa la kisiasa kufanya hivyo, badala yake akemee katika mimbari yake kwa maana msikitini au kanisani.”

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Dini ya Kiislamu Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha alisema ingawa siasa na dini ni vitu vinavyochangamana, utekelezwaji wake ni tofauti.

Alisisitiza ni sahihi kiongozi wa dini kukosoa mabaya yanayofanywa na kiongozi wa Serikali, lakini si kwa kutumia jukwaa la siasa.

Alikemea pia matumizi ya jukwaa la kisiasa kutengeneza mkanganyiko baina ya waumini ambao aghalabu huwa na itikadi tofauti.

Hata hivyo, suala hilo linatajwa kuwa kinyume na haki ya kikatiba inayompa uhuru kila mwananchi kushiriki siasa, kama inavyofafanuliwa na Mchungaji Peter Msigwa.

Mchungaji Msigwa, na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini, alisema haoni shida ya kuwa kiongozi wa dini, huku anashiriki siasa kwa kuwa ni haki yake ya kikatiba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live