VYAMA vya siasa vya upinzani vimesema siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan zimekuwa za faraja na matumaini kwa Watanzania.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, John Shibuda alisema katika siku 100, serikali ya Rais Samia ilijitahidi kutafuta majibu ya changamoto zinazowakabili Watanzania.
Shibuba alisema serikali ya Awamu ya Sita ilichambua mambo ya serikali zilizotangulia na kufanya maboresho ili kuboresha maisha ya wananchi na kuinua uchumi wa nchi.
“Wafanyakazi Tanzania ni mashujaa wetu kwa michango yao iliyotumika kujenga miradi ya kimkakati, hawa watu ni mashujaa ambao wamejitoa mhanga kama wazee wetu walivyojitoa muhanga kwa damu zao kudai uhuru, kwa hiyo wafanyakazi wa Watanzania watazamwe kwa jicho la pekee na la huruma,”alisema,
Shibuda alisema kaulimbiu ya Rais Samia kwamba ‘Kazi Iendelee’ imetekelezwa kwa vitendo kwenye maeneo mbalimbali ukiwemo ujenzi wa miradi mikubwaya kimkakati.
Pia alisema katika siku 100, Rais Samia ameonesha uimara na umadhubuti wa kukiongoza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kukirejesha katika mfumo wa kuwa na vikao hai kwa mujibu wa matakwa ya Katiba ya CCM.
“Serikali ya Awamu ya Sita pia imetengeneza taswira mpya duniani kuhusu haki ya uhuru wa habari na Waziri Mkuu ameendelea kusisitiza kuhusu uhai wa uhuru wa habari, haki za kiraia za kutoa maoni bila hofu,Samia pia ameunda diplomasia ambayo ni chambo cha kunasia wawekezaji, kwa hiyo Awamu ya Sita imeng’arisha sumaku ya kuvutia imani ya wawekezaji,”alisema Shibuda.
Alisema serikali ya Samia iko katika dira ya ndoto ya waasisi wa taifa kuiwezesha nchi kujitegemea kiuchumi ndiyo maana anawahimiza Watanzania walipe kodi, wawe waaminifu na wazalendo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Magdalena Sakaya alisema uongozi wa Rais Samia umeonesha dhamira ya kuwapa watu matumaini na faraja.
“Pia ningemshauri asimamie sana uwajibikaji na utendaji ili kuleta nidhamu kwenye utendaji, asimamie kwa karibu matumizi ya fedha ili iwepo nidhamu ya matumizi hayo, afanye kazi na vyama vya siasa kwa sababu siasa ni sehemu ya maisha ya Watanzania, aviite vyama vya siasa aongee nao ili washirikiane na serikali kikamilifu katika kujenga taifa letu,”alisema Sakaya.
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia amepongeza jitihada za Rais Samia kuimarisha makusanyo ya kodi.
”Kati ya mambo ambayo ameanza kuyafanya mazuri ni pamoja na hili la kodi, huyu Rais ameonesha kuwa hataki kodi za dhuluma na hapo amefanya jambo jema kati ya mengi, ila bado kuna kero ambazo NCCR- Mageuzi inaona kuwa bado zinatakiwa kufanyiwa kazi.”alisema Mbatia Dar es Salaam.
Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, ana imani kuwa Rais Samia atakutana na wanasiasa kutoka vyama vya upinzani ili kujadili namna ya kukabiliana na kero katika jamii.
“Mimi ninaona kuwa kuna mambo mengi ambayo tunapaswa kuzungumza na Rais Samia na akitupatia muda tunajadiliana kwa faida ya nchi hii, kwa kuwa amesema anataka kubadilisha nchi tukutane kujadili njia salama za kuboresha ujenzi wa nchi.”
Kuhusu ugonjwa wa Covid-19 Mbatia alisema kuna haja ya kuongeza uwekezaji kwa kuongeza vituo vya upimaji.
Pia alishauri kupunguzwa kwa tozo ya upimaji wa corona hasa kwa Watanzania wanaokwenda nje ya nchi.