Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ataka kadi za kielektroniki za CCM kuwafikia wanaostahili

581952e477e9644130b9a56242b544ee Ataka kadi za kielektroniki za CCM kuwafikia wanaostahili

Sun, 27 Feb 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Abdulla Juma Sadalla amewataka viongozi wa chama Wilaya ya Kusini Unguja kuhakikisha kadi mpya za uanachama za elektroniki zinawafikia wanachama wote wenye sifa na vigezo vya kupata kadi hizo.

Wito huo aliutoa katika hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa kadi hizo katika Wilaya ya Kusini Unguja.

Alisema lengo la kadi hizo ni kuwafikia walengwa kwa haraka ambao ni wanachama ili zitumike katika shughuli mbalimbali za chama.

Alieleza kuwa CCM ni taasisi ya kisiasa inayoenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, ndio maana ikaweka mfumo imara wa kadi za kisasa zinazohifadhi kumbukumbu zote za wanachama wa CCM.

“Matarajio yetu ni kuwa kadi hizi hazitokaa maofisini mwenu, hakikisheni kila mwanachama anayestahili kupata kadi anapewa bila vikwazo,” alisisitiza.

Katika maelezo yake, Dk Sadalla alieleza kuwa ugawaji wa kadi hizo ni mwendelezo wa shughuli za uzinduzi wa kadi uliotekelezwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais Samia Suluhu Hassan katika kilele cha kuadhimisha kutimiza miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM kilichofanyika mkoani Mara.

Kupitia hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo aliwasihi wanachama, viongozi, watendaji na makada wa CCM kuhakikisha wanazitunza vizuri kadi hizo kwani uzalishaji wake ni gharama kubwa.

Akizungumzia uchaguzi mkuu wa chama, Dk Sadalla aliwakemea baadhi ya wanachama walioanza kutengeneza makundi ya kukigawa chama na kuwafanyia kampeni za siri baadhi ya watu wakati bado viongozi wa chama na serikali hawajamaliza muda wao wa uongozi.

Sadalla akizungumzia Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka huu 2022, aliwasisitiza wanachama na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa ili serikali iweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa takwimu sahihi ya watu na demografia.

Alikemea vitendo vya udhalilishaji na kuwataka wanachama na wananchi wa Wilaya ya Kusini kupinga vitendo hivyo na kuhakikisha wanaendelea kuishi katika maadili, mila na desturi sahihi za Kizanzibari.

Katika hatua nyingine, Dk Sadalla alikemea tabia za baadhi ya wananchi wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kukosoa na kubeza kwa kejeli hatua za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Zanzibar.

“Kuna kundi linatumia mitandao ya kijamii kubeza juhudi kubwa za maendeleo zinazofanywa na serikali yetu, tunajua lengo lao ni kudhohofisha juhudi hizo na sasa tunawaambia hatuwezi kurudi nyuma ni mwendo wa kasi hadi 2025,” alisema.

Kupitia kikao hicho aliwapongeza WanaCCM wote walioshiriki katika uzinduzi wa sherehe za miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika wilayani humo.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Amina Imbo, alisema walipokea kadi mpya 4,000 na Wilaya ya Kusini Unguja wamepewa kadi 1,782 wakati Wilaya ya Kati walipewa kadi 2,218.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Asha Mzee alisema wanachama wote ni 14,484 ambapo waliosajiliwa awali ni 8,800 na usajili mpya ni 1,140 na waliosajiliwa mpaka sasa ni wanachama 9,940.

Akieleza kazi za serikali ya Zanzibar ya awamu ya nane, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Rahma Kassim Ali ambaye ni mwakilishi wa Viti Maalumu Mkoa wa Kusini Unguja alisema tayari serikali imekwishamaliza kufanya upembuzi yakinifu barabara za ndani zenye urefu wa kilomita zaidi ya 200 ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami.

Alisema katika barabara hizo tayari wapo eneo la mradi kwa ajili ya kumalizia michoro ya ujenzi wa barabara hizo.

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Umwagiliaji na Mifugo, Soud Nahoda Hassan ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Paje alisema tayari serikali imekwishaanza utafiti kwa ajili ya matumizi bora ya mbolea za asili na wamefanya hivyo baada ya kubaini kuwa mbolea za kisasa zinachangia maradhi mengi ya binadamu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz