Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asilimia 75 vijana ACT-Wazalendo kugombea nafasi mbalimbali

99055 Pic+act Asilimia 75 vijana ACT-Wazalendo kugombea nafasi mbalimbali

Fri, 12 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu

Asilimia 75 ya waliojitokeza kuwania nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kupitia Chama cha ACT-Wazalendo ni vijana katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Kampeni na Uchaguzi Taifa kutoka chama hicho, Mohammed Massaga, na kudai kuwa hamasa hiyo ya vijana kujitokeza inaashiria muamko mkubwa katika siasa za Tanzania kwa vijana na ari ya kuliletea Taifa maendeleo.

“Katika majimbo 120 ya Tanzania asilimia 75 wamejitokeza vijana kwa hio hali ni nzuri katika kuonyesha muamko na msisimko wa kisiasa kwa sasa” amesema Massaga

Mwenyekiti wa Chama hicho na mwanasiasa mkongwe, Maalim Seif akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam juzi licha ya kueleza vikwazo 10 kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba alisema kuwa ACT-Wazalendo haifikirii kususia uchaguzi huo.

Muamko wa aina hiyo kwa vijana umeonekana pia kwa Chama Kikuu cha Upinzani nchini, Chadema na kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama hicho (Bavicha), John Pambalu Vijana zaidi ya 500 wamejitosa kuwania nafasi za ubunge na udiwani kupitia chama hicho.

Mmoja wa Vijana kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye amejipanga kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo mojawapo nchini, John Jilili akizungumza na The Guardian Digital kuhusu mwamko huo wa vijana katika siasa za Tanzania amewataka vijana kujitokeza kupiga kura kuliko kuishia kufanya siasa za kwenye mitandao ya kijamii.

“Tatizo la baadhi ya vijana wengi wanaishia katika mitandao ya kijamii tu bila kuchukua hatua nyingine za ziada kama kupiga kura” amesema Jilili.

Jilili amewataka vijana kuwa mstari wa mbele kuhamasishana katika kuwania nafasi za uongozi kwa kile alichoeleza kuwa maendeleo ya Taifa lolote huwategemea zaidi vijana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live