Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aomba Uwanja wa Nyamagana uitwe Magufuli

D7b1f5819c01672894396f3ba4562ac8.jpeg Aomba Uwanja wa Nyamagana uitwe Magufuli

Sat, 20 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

DIWANI wa kata ya Nyamagana ambae pia ni Naibu Meya mstafu wa jiji la Mwanza,Bhiku Kotecha ameiomba Halmashauri ya jiji la Mwanza ibadilishe jina uwanja mkongwe wa Nyamagana na kuuita jina la Magufuli ikiwa ni heshima ya kumbukumbu ya Rais Magufuli aliyefariki dunia Jumatano ya wiki hii.

Kotecha alisema Rais Magufuli alisimama imara katika kuhakikisha uwanja wa Nyamagana hauuzwi pamoja na upatikanaji wa nyasi bandia zilizokua zimezuiliwa bandarini Dar es Salaam.

“Rais alitoa onyo kali kwa atakaeuza uwanja wa Nyamagana atamfunga jela, kiukweli rais aliupigania sana uwanja wetu,’’alisema Kotecha.

Katibu mkuu wa Chama cha soka Mwanza (MZFA),Leonard Malongo alisema atamkumbuka rais Magufuli kwa mipango yake ya kuhakikisha anaboresha miundo mbinu ya michezo ikiwemo mpango wa kujenga uwanja mkubwa wa Dodoma.

Alisema rais Magufuli aliwahi kutembelea uwanja wa Nyamagana Julai 2017 na kushuhudia mechi ya ligi daraja la nne kati ya Nyamwagwa FC dhidi ya Buhongwa.

Alisema aliboresha baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kujali michezo yote na sanaa.

Kocha wa timu ya Watengwa FC,Godfrey Alfred alisema Rais Magufuli kupitia sera yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ imegusa taasisi nyingi nchini na Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF)limekuwa na nidhamu kubwa ya fedha.

Alisema wakati Rais Magufuli anaingia madarakani TFF ilikuwa na hati chafu kutoka Shirikisho la soka la kimataifa, FIFA jambo lililosababishwa kutopata mgao wa Fifa kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo.

Rais wa mpira wa Kikapu nchini (TBF),Phares Magesa alisema watamkumbuka Rais Magufuli kwa kuwa katika kipindi chake viwanja mbalimbali vya mchezo wa mpira wa kikapu vilijengwa ikiwemo uwanja wa Mirongo na Sabasaba vilivyopo Mwanza.

Alisema pia uwanja wa mchezo huo ulijengwa katika mkoa wa Simiyu na mashindano ya Taifa yakafanyika katika mkoa huo kwa mara ya kwanza.

Chanzo: www.habarileo.co.tz