Mbunge wa Same Mashiriki (CCM), Anne Kilango amelalamikia baadhi ya wakazi wa kata ya Kihurio kwenye jimbo lake kudanganywa kuhusu changamoto ya maji na kupewa maneno ya kumchafua mbunge na Serikali.
Kilango ameyasema hayo leo Jumanne Novemba Mosi 2022 wakati akiuliza swali la nyongeza bungeni.
Amempongeza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuwa ametatua tatizo la maji katika kata ya Bendera lakini matatizo kwenye kata ya Kihurio yamezidi kuwa mabaya.
“Sasa wananchi wengine wanadanganywa na kupewa maneno ya kumchafua mbunge na Serikali. Waziri utaniambia nini kuhusu matatizo ya maji katika kata ninayotoka mimi?”amehoji.
Akijibu, Aweso amemuagiza Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) wa mkoa wa Kilimanjaro kwenda haraka kulitatua tatizo hilo ili wakazi hao waweze kupata maji.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khanani amesema changamoto kubwa inayolikumba Taifa katika maji ni kwasababu Serikali inatumia mabwawa ambayo yanategemea mvua kupata maji.
“Ni lini Serikali mtaanza kutumia maziwa makuu kama vyanzo vya maji kuliko kutegemegea vyanzo vya hivi sasa,”amesema.
Akijibu swali hilo, Aweso amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kutumika kwa raslimali toshelevu katika kuhakikisha anamtua mama ndoo kichwani.
Amesema Wizara ya Maji inatekeleza hilo kwa kutumia raslimali toshelevu hususan maziwa na mito mikubwa ili kuhakikisha Watanzania wanapata maji.