Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anachokisema Heche kuhusu utekelezaji wa bajeti

51738 HECHE+PIC

Thu, 11 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche amesema utekelezaji mdogo wa bajeti kuu ya Serikali ya Tanzania unakwamisha kukamilika kwa miradi ikiwamo kilimo kinachoajiri idadi kubwa ya wananchi.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 11, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) mwaka 2019/20.

Amesema katika afya bajeti iliyopita zilitengwa Sh561 bilioni lakini zilizopelekwa hadi sasa ni Sh89 bilioni na hakuna dawa wala nyuzi.

“Mnasema nyinyi ni Serikali ya viwanda wakati mlitenga Sh90 bilioni fedha ambazo zimekwenda kwa ajili ya maendeleo ya viwanda ni Sh5.4 bilioni yaani asilimia sita peke yake,” amesem Heche na kuongeza:

“Ndio maana mnasema vyerehani vitano ni kiwanda, kama mmetenga Sh90 bilioni na zinakwenda fedha kiasi hicho kwa nini msiseme kiwanda cha vyerehani vitano visiwe kiwanda au cha gongo nacho ni kiwanda.”

Amebainisha kuwa katika kilimo kinachoajiri asilimia 70 ya  Watanzania, kutoa chakula kwa Watanzania asilimia 100 na malighafi za viwandani asilimia 80, kilitengewa Sh98.1 bilioni lakini zilizotolewa ni Sh42 bilioni.

Kuhusu mfuko wa maji amesema: “Mfuko wa maji tulipitisha hapa kwa mbwembwe mkapiga na makofi Sh299 bilioni ila fedha zilizokwenda kwenye mfuko huo ni Sh1 bilioni.”

Kauli hiyo ya Heche imemnyanyua naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na kusema: “Katika bajeti ya mwaka jana tulitengewa Sh158 bilioni mpaka Februari tumepokea zaidi ya Sh93 bilioni, nimuombe ajiridhishe asipotoshe Bunge.”

 

Heche akijibu taarifa hiyo ya naibu waziri amesema hazungumzii fedha kutoka kwa wahisani, anachozungumzia ni fedha za mfuko wa maji: “Waziri anajua ninachozungumza, kama tutakuja hapa bungeni kupitisha bajeti ambayo utekelezaji wake ni chini ya asilimia 30 sasa tunapitisha bajeti ya nini.”

Kuhusu utendaji wa halmashauri amesema: “Sehemu ambayo Serikali inakutana na shida za watu kila siku ni katika halmashauri zetu, ndizo zinazosimamisha shule ambazo watoto wa wananchi maskini wanasoma, hakuna mbunge ambaye atasimama hapa na kusema mtoto wake anasoma shule hizi za Serikali.”

“Hospitali zinasimamiwa na halmashauri, nianze na halmashauri ya Tarime, hii ina mwezi wa nne vikao vimesimamishwa kinyume cha utaratibu wa kisheria, eti kwa kisingizo cha ufisadi umefanyika, kama wapo waliofanya ufisadi mkuu wa mkoa achukue hatua kwa hao mafisadi si kuzuia vikao.”

Pia, amesema baraza la madiwani halikutani: “Kuna watoto  1,030 wameshindwa kwenda sekondari kwa sababu hakuna  madarasa. Tumetenga zaidi ya Sh250 milioni tunazo hizi fedha zipo katika akaunti ila mkuu wa mkoa amezuia vikao kukaa, anataka tumwandikie barua kumuomba fedha wakati Bunge ndilo linalogawa fedha.”

Mbunge huyo amehoji sababu za vikao hivyo kuzuiwa wakati polisi wakiendelea na kazi licha ya kutajwa kwa ufisadi katika taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad inayoishia Juni 30, 2018.



Chanzo: mwananchi.co.tz