Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amina Mollel; Mwanahabari aliyejitosa bungeni kusaidia jamii

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. “Nilitamani siku nyingi kuwa mbunge na wakati ulipofika sikuona haya kugombea nitimize ndoto zangu, nashukuru Mungu nilithubutu na sasa nawawakilisha wanawake wenye ulemavu bungeni,”

Ndivyo Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mkoa wa Arusha Amina Mollel alivyoanza kuzungumza na Mwananchi wakati akielezea nafasi ya wanawake katika kusimama na kuhakikisha wanatimiza ndoto zao bila woga.

Amina ni kati ya wanahabari wachache waliofanikiwa kupenya kwenye siasa na kushika nafasi ya uongozi hasa ubunge.

Kati ya habari zilizombeba wakati akifanya kazi katika Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ni makala iliyomsaidia mwanamke mwenye ulemavu, wilayani Makete mkoani Njombe, Sara Mageni kupewa bajaj na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

“Habari za kijamii ndizo ninazozipenda zaidi, hata sasa nikipata nafasi nitaziandika hizo,” anasema.

Mbunge huyo kila anapopata nafasi ya kuzungumza bungeni amekuwa akiwaongelea watu wenye ulemavu, hasa katika kuona wanapata haki zao kama ilivyo kwa wengine.

Amina anasema anaamini kweli elimu. “Nimefika hapa nilipo kwa sababu wazazi wangu walitambua umuhimu wa elimu, waliwekeza kwenye elimu. Ukimsomesha mlemavu hautapata hasara ila utapunguza mzigo,” anasema na kuongeza:

“Kila siku huwa napenda kutumia mfano wa Maria na Consolata, watoto hawa walikuwa walemavu na waliivutia dunia kwa sababu walezi wao waliwekeza kwenye elimu.”

Anasema kiuhalisia licha ya elimu, kundi hilo linahitaji miundombinu salama na wezeshi.

“Lakini wanawake walemavu wanahitaji kuheshimiwa zaidi, kusimamiwa na kusaidiwa wafikie malengo yao,” anasema.

“Naiamini taaluma ya habari kwa sababu hiyo ndiyo imenikuza na hivi sasa nimepata ubunge,” anasema.

Amina ambaye ni miongoni mwa wanahabari wanachama wa Chama Cha Waandishi wa Habari Tanzania (Tamwa) anasema harakati alizowahi kufanya kupitia chama hicho katika kupinga ukatili wa kijinsia, pia zilimsaidia kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake, na hivyo kuwa rahisi kuzifanyia kazi bungeni.

Anasema waandishi wa habari wanawake wanayo nafasi kubwa ya kutumia peni ili kufikia malengo wanayoyataka.

Kujituma, bidii, uaminifu na uthubutu ni kati ya vitu vilivyomsaidia kutimiza ndoto yake ya kuwa mbunge ili apate nafasi ya kuwatetea watu wenye ulemavu na wanahabari wenzake.

“Wapo baadhi ya watu wakiwaona wanawake wanashika nafasi za juu za uongozi wanadhani wamebebwa au la wametumia miili yao ‘ngono’ kufikia hapo walipo, hapana,” anasema.

Anasema ikiwa mtu atajituma na kuthubutu ni rahisi kufika mahali popote anapotamani kupafikia.

Anawashauri wanawake kujiamini na kujiendeleza kielimu, kwa madai kuwa moja ya sababu za kuwaangusha chini ni kiwango kidogo cha elimu.

Anasema ipo haja ya wazazi kuwahimiza watoto wao wa kike kusoma kwa bidii, ili ufaulu wao iwe silaha kubwa ya kutimiza ndoto zao.

“Ikiwa mtoto atafaulu na atafikia mbali kielimu, ni rahisi kutimiza ndoto ya kuwa yeyote anayetaka. Kitu pekee kinachotuangusha zaidi ni kiwango kidogo cha elimu, ukiwa na elimu ndogo hutaweza kuingia kwenye nafasi za kiuongozi za juu kama ubunge na nyingine. Tuwekeze kwenye elimu,” anasema.

Hata hivyo anataja vitu vingine ambavyo vimekuwa vikiwarudisha nyuma wanawake kuwa ni chuki, roho mbaya na ubinafsi.

Anasema wapo baadhi yao wanawake waliofanikiwa kufika mbali, lakini badala ya kuwapandisha wenzao, wamekuwa wakiwasukuma ili waanguke.

“Tuache chuki, roho mbaya na ubinafsi. Kazi kubwa kwetu sisi wanawake tulioweza kufika tulipo iwe ni kushikana mikono na kuwavuta wengine wafikie ndoto za mafanikio yao kama sisi,” anasema.

tulivyoweza kufikia,” anasema.

Kuhusu taaluma ya habari

“Kalamu ni kama njiti moja ya kiberiti ambayo ikiwashwa inaweza kuchoma msitu mkubwa. Kalamu inapotumika vema ina mchango mkubwa kwenye jamii, inaweza kuleta mabadiliko chanya na kuongeza uwajibikaji,’ anasema.

Anasema waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kutumia ipasavyo kalamu zao kuisaidia jamii.

Anasema yeye alitimiza wajibu wake wakati alipokuwa kazini na bado anaendelea kuifanya kwa sababu anaamini, taaluma ipo ndani mwake.

“Nafikiria kuendelea kuandaa vipindi vyenye kuielimisha jamii kwa sababu licha ya ubunge wangu, mimi ni mwanahabari,” anasisitiza.

Anawaasa wanahabari kuwasemea watu wasio na uwezo wa kusema hasa vijijini ili Serikali iwajibike kupitia changamoto watakazoibua.

Anasema inawezekana kuna jamii haina uhakika wa maji safi na salama, lakini Serikali haijui hivyo kupitia kazi ya mwandishi, wahusika wanaweza kuwajibika na wananchi wakapata huduma wanayoipenda.



Chanzo: mwananchi.co.tz