Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyoyafanya zelothe CCM enzi za uhai wake…

Zelothe Stephenrre Alama alizoacha Zelothe CCM

Sat, 28 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Arusha. Viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wameeleza kifo cha Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Zelothe Stephen ni pengo na atakumbukwa kwa kupenda umoja, ushirikiano na aliyechukia makundi.

Zelothe alifariki dunia juzi, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam na maziko yanatarajiwa kufanyika keshokutwa, huku mwili wake ukitarajiwa kupelekwa Arusha leo.

Zelothe kabla ya kuwa Mwenyekiti wa CCM, aliwahi kuwa Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Wilaya ya Musoma.

Alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha Desemba 2019 na alifanikiwa kutetea kiti hicho katika uchaguzi uliofanyika Novemba, 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Seipulani Ramsey alisema mwili wa kiongozi huyo utapokewa leo alasiri katika uwanja wa ndege Arusha na utapelekwa hospitali ya Mount Meru.

"Tunaomba wana-CCM wote Mkoa wa Arusha kujitokeza uwanja wa ndege kupokea mwili wa mwenyekiti wetu na Jumatatu kuja katika mazishi," alisema.

Alisema maziko yatafanyika Kata ya Olorieni katika kijiji cha Olosiva, wilayani Arumeru.

"Tuendelee kumuenzi Mwenyekiti wetu alipenda sana umoja na ushirikiano, aliyechukia makundi," alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa ya Jumuiya ya wazazi wa CCM mkoa Arusha, Moses Adam, alisema Zelothe atakubukwa kwa kuwaunganisha wana-CCM.

"Zelothe alikuwa ni kiongozi mkweli, alikuwa hapendi makundi na alikipenda chama chetu," alisema.

Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mussa Matoroka alisema atamkumbuka Zelothe kwa kuwa kiungo kizuri baina ya CCM na Serikali pamoja na vyombo vingine vya usalama.

"Alikuwa kiongozi makini, mchapakazi na mzalendo," alisema.

Katibu wa uenezi mstaafu wa CCM mkoani hapa, Gerald Munisi alisema, "Tumepokea kwa masikitiko msiba huu, tumempoteza kiongozi mahiri wa CCM na ameshika nafasi nyingi serikalini."

Naye Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba alisema chama hicho kimepoteza kada wake shujaa, aliyekipenda tangu akiwa mtumishi wa Serikali, akifanya kazi katika Jeshi la Polisi.

Alisema kitu ambacho Zelothe hakufanya ni kutovua magwanda ya Polisi na kuvaa ya CCM, lakini chama hicho kilikuwa kwenye moyo wake.

Makamba alisema Zelothe alidhihirisha kuwa anaipenda CCM kwa sababu alipostaafu tu, alikwenda kugombea uenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Rukwa na akashinda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live