Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyempeleka Upendo Peneza Chadema ni huyu

Snapinsta Peneza Aliyempeleka Upendo Peneza Chadema ni huyu

Tue, 21 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbunge wa zamani wa Chadema (2015-2020) ambaye sasa amehamia CCM, Upendo Peneza ameeleza namna Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf alivyomshauri mambo matatu kabla ya kuhamia chama tawala.

Hata hivyo, Peneza ambaye alikuwa mwekahazina wa Chadema, Kanda ya Victoria inayojumuisha mikoa ya Geita, Mwanza na Kagera, amesema haikuwa kazi rahisi kufikia uamuzi huo kwani alifunga na kuomba ili kufanikisha hilo.

Mwanasiasa huyo alihamia CCM Januari 22, 2024 akieleza amevutiwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya chama hicho tawala.

Peneza ameeleza hayo leo Jumatatu, Mei 20, 2024 wakati wa mahojiano maalumu alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL), zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

Katika mahojiano hayo Peneza amezungumzia pia safari yake ya kisiasa alipotoka hadi alipo sasa.

“Nakumbuka nilimtafuta ‘mentor’ wangu mmoja (Sirleaf), nilikubaliane naye tukakutana Dubai, tukazungumza, nikamueleza na hakuona wazo langu baya, lakini alinishauria mambo matatu,” amesema Peneza.

Sababu Peneza kuhamia CCM

Katika maelezo yake, Peneza amesema aliambiwa na Sirleaf ahakikishe kama kweli ameamua kuhamia CCM, basi uamuzi huo uwe imara na asiwafanyie mzaha wananchi kwamba leo yupo huko kesho kule.

“Aliniambia nipime nilipo, ninapotaka kwenda kwa kuhakikisha nafanya uamuzi imara, jingine aliniambia nihakikishe watu wangu (wawakilishi) niliokuwa ndani ya Chadema wanielewe vizuri.

“Pia alinitaka kutafakari vizuri namna gani nasonga mbele zaidi, kwamba nafanya uamuzi halafu? Vyote nilivifanyika kazi kabla sijahama, namshukuru sana, uamuzi niliofanya sikuufanya tu kama mwanamke ambaye ana msongo wa mawazo,” amesema Peneza.

Peneza amebainisha kuwa alimfahamu Sirleaf alipokuwa mbunge na walikutana kwenye moja ya mikutano ya kimataifa na alivutiwa naye na kumfanya kuwa mshauri wake.

“Ni mtu ambaye huwa tunazungumza mara kwa mara, hata baada ya uchaguzi wa mwaka 2020, nilikwenda Liberia tukaongea na kunipa ushauri wa kisiasa, amekuwa na mimi katika nyakati hadi wa kufanya uamuzi,” amesema Peneza.

Peneza amesema alimuomba Mungu kwa siku nyingi ili amsaidie katika uamuzi huo, sambamba na kushirikisha watu wake wa karibu wakiwemo marafiki, asasi za kiraia walioamlea pamoja na familia yake waliompa baraka.

“Niliwaambia viongozi (wa Chadema) pia nimefika hatua moyo wangu umetoka katika hii taasisi, haupo tena Chadema, tukaenda mbele nikawaeleza nimebakisha akili na nguvu tu.

Akizungumza na waandishi wa Mwananchi leo jijini Dar es Salaam

“Nikawaambia tena kwa sasa akili yangu nimeitoa na kubakisha nguvu tu ambayo haikuwa na kazi tena, katika hatua kubwa katika maisha yangu ya kisiasa ni kuhama Chadema,” alisema.

Amewataka Watanzania kumuelewa kuwa yeye sio mtu wa kuchezea hisia na imani zao, akisema anawathamini kwa sababu walimpa imani akiwa bado mdogo katika safari yake siasa.

Aitaka Chadema ijitakafari

Katika hatua nyingine, Peneza ameishauri Chadema ijitafakari akisema inaweza kufuata historia ya vyama vya NCCR-Mageuzi na CUF vilivyowahi kuongoza kambi ya upinzani nchini.

Amedai dalili za chama hicho kusambaratika zimeonekana kutokana na kauli za baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho kutuhumiana kwa rushwa, huku wengine wakidaiwa kuhongwa maarufu kama kulamba asali.

Mei 2 mwaka huu, akiwa mkoani Iringa, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu alitoa madai ya uwepo wa fedha zilizomwagwa kwenye uchaguzi wa ndani wa Chadema.

Katika hotuba yake siku hiyo Lissu alisema: “Wakati nakuja hapa Iringa jana na juzi kulikuwa na mtafaruku mkubwa sana, sijui kama mnafahamu, ndani ya chama chetu kuna pesa nyingi ajabu kwenye uchaguzi huu.

“Leo kwenye uchaguzi kuna hela ya ajabu, ninyi mnafikiri hiyo hela ni ya wapi? Mnafikiri hiyo hela ni ya nani? Mnafikiri hiyo hela itatuacha salama? Ukitaka kujua kwamba hatuko salama, fuatilia mitandaoni,” alisema Lissu.

Kutokana na kauli hiyo na nyinginezo, Peneza amesema Chadema ina nafasi ya kujisahihisha.

“Chadema wana nafasi ya kuangalia wenzao (CUF na CCM), wamekosea wapi ili kujisahiisha, chunguza hivyo vyama vilianza kushutumiana rushwa, viongozi kugawanyika na kutokuwa na timu moja katika kufanya kazi.

“Mwishowe wao (Chadema) na wanachama wana jukumu kuandamana kuelekea ofisi za Chadema kudai chama chao, ambacho zamani kilikuwa na uwezo wa kuusema ufisadi, hakijawahi kutuhumiana rushwa hadharani na kilikuwa na sauti katika jamii,” amesema

Amewataka wanachama wa Chadema kuandamana kwenda katika ofisi za chama hicho ili kuwauliza viongozi wanakosea wapi kwa lengo la kujisahihisha.

“Pamoja na kwamba nimeondoka, lakini ninaamini katika upinzani nchi inatakiwa kuwa na upinzani imara, sasa Chadema wajiangalie ndani, wanakosea wapi au wanavuruga wapi ili kujirekebishe na kujisahiisha.

“Inawezekana binadamu ukaenda ukapata kiburi kichwani, kwamba mimi ndio chama kikuu cha upinzani nchini, ukipata kiburi na kusahau misingi na mizizi iliyokufanya uwe juu maana yake unakaribisha anguko,”amesema Peneza.

Peneza amesema ni jukumu la Chadema kukubali kukosolewa kwenye upungufu na sio kumtukana badala yake wayafanyie kazi kwa manufaa ya Taifa kwa sababu vyama vya siasa vinapokea ruzuku ya Serikali.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana kuhusu kauli za Peneza, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, amesema hakuna kada wa CCM anayekitakia mema chama chake, bali wanakitakia mabaya.

“Peneza angekuwa anakipenda Chadema, asingeondoka, ameshindwa kuitetea CCM ndio maana kila kukicha ni Chadema tu. Hatujamfukuza ameondoka mwenyewe.

“Kwa sasa Chadema tumejikita katika kuangalia uchaguzi wa kanda nne utakaoanza Mei 25 mkoani Kagera,” amesema Mrema akizungumza na Mwananchi.

Utendaji wa Rais Samia

Peneza amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi anayejitahidi kurejesha demokrasia ya nchi na kuleta mageuzi makubwa ndani ya jamii yetu. Amesisitiza Rais Samia anaangalia mambo mema na kuyapambania.

“Rais Samia ni kiongozi mvumilivu, anayejitambua na yuko tayari kuleta mageuzi katika Taifa hilo amelitekeleza kwa kiasi kikubwa katika sekta za afya, kilimo na kuinganisha Tanzania na mataifa mengine,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live