Aliyekuwa mgombea wa uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Morogoro, Nasoro Duduma amesema uchaguzi huo uligubikwa hila mbalimbali zilizofanywa na baadhi ya Wanaccm ikiwemo rushwa.
Duduma amesema kutokana na vitendo hivyo, ndio maana wajumbe walibadilika ghafla ukumbini na kuamua kumchagua mgombea mwenzake, Joseph Masunga.
Uchaguzi huo ulimalizika jana Jumatatu, Novemba 21, 2022 ambapo Duduma alishindwa uchaguzi huo kwa kupata kura 448 huku mwenzake Masunga akipata kura 621.
Alisema pamoja na kushindwa uchaguzi huo ambao ulikuwa na wapigakura 1,207 anakubali matokeo hayo na sasa ataendelea kuwa kada na mwanachama mtiifu.
"Nilipoingia kwenye uchaguzi niliamini ninaweza kukiongoza chama kwa kuwa nipo ndani ya chama kwa muda mrefu hivyo nina uzoefu wa kutosha, tathimini yangu kabla ya wajumbe kuingia ukumbini ilionesha nina nafasi kubwa ya kushinda lakini ghafla wajumbe wamebadilishwa na kuamua waliyoamua kwenye sanduku la kura," alisema Duduma.
Aidha, Duduma alisema uchaguzi huo ulikuwa na vyombo vikubwa vya uangalizi hivyo anaamini hila zote zilizofanywa ndani na nje ya ukumbi zimeonekana na vyombo hivyo.
Aliwashukuru wajumbe waliompigia kura na wale wasiompigia kura na kusema kwa sasa yuko tayari kuwaunga mkono wote waliochaguliwa katika nafasi mbalimbali katika kukiimarisha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.
Katika uchaguzi huo, Jonas Nkya alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) kwa kupata kura 932.
Kwa upande wake, Masunga ambaye amechukua nafasi ya Dorothy Mwamsiku ambaye jina lake lilikatwa alisema atahakikisha anatenda haki katika kipindi chote cha Uongozi wake wa miaka mitano.
Katika uchaguzi huo, mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa anayewakilisha mkoa wa Morogoro amechaguliwa Jonas Nkya.
Jana Jumatatu, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma alisema, wanafuatilia vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo vitendo vya rushwa.
Chongolo alitoa kauli hiyo baada ya kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mkoa wa Simiyu pamoja na kusimamisha uchaguzi wa wajumbe wa halmashauri kuu mikoa ya Arusha na Mbeya.