Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alichokisema Meya wa Chadema Iringa anayedai kutaka kung’olewa

97738 Pic+meya Alichokisema Meya wa Chadema Iringa anayedai kutaka kung’olewa

Mon, 2 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa/Dar. Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe amesema amepokea barua ya mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa akitakiwa ndani ya siku tano kujibu tuhuma zinazomkabili ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Machi 2, 2020 mjini Iringa Kimbe amesema, “nimepokea  barua ina tuhuma nne ambazo ni matumizi mabaya ya madaraka, matumizi mabaya ya rasilimali za Halmashauri, mwenendo mbaya au ukosefu wa adabu na kushiriki katika vitendo vya rushwa.”

Amesema alipaswa kupokea barua ya tuhuma hizo pamoja na majina ya madiwani 19 ambao wameunga mkono hoja tajwa, kubainisha kuwa tuhuma hizo ni za kupangwa na hazina ukweli wowote.

“Kwa mujibu wa barua hii ninatakiwa niijibu ndani ya siku tano, kesho nitapeleka barua kwa mkurugenzi nikimweleza na kumkumbusha vyombo vya usalama na watendaji wake taratibu na kanuni za kumtoa meya madarakani wamezikosea ”amesema.

Meya huyo ameeleza kuwa lengo la kupeleka barua hiyo ni kutaka kupewa nakala ya majina ya madiwani waliosaini hoja hiyo na kuomba ushahidi wa kila tuhuma ili ajibu.

 “Nimekusudia kwenda mahakamani kuzuia mchakato huu haramu wa kutaka kuniondoa madarakani iwapo Mkurugenzi hatonipa majibu ya kuridhisha,  sote tunajua CCM imekosa fursa ya kwenda kwa wananchi badala yake wanadhani kununua madiwani wataweza kulikomboa  jimbo,” amesema.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Kimbe amepewa siku tano kujibu tuhuma zinazomkabili ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka.

Hatua hiyo imefika baada ya wajumbe 19 wa Baraza la Madiwani la manispaa hiyo, kusaini maombi wakitaka kifanyike kikao maalum cha kujadili kumng’oa madarakani.

Kulingana na barua iliyosainiwa leo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Hamid Njove meya huyo anatakiwa kuwasilisha utetezi wake kwenye ofisi za mkurugenzi huyo ndani ya siku tano kuanzia leo.

Miongoni mwa tuhuma zinazomkabili Kimbe ni matumizi mabaya ya madaraka ikiwamo kufanya maamuzi bila kuzingatia kanuni za kudumu za Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Tuhuma nyingine ni matumizi mabaya ya rasilimali za halmashauri hiyo ikiwamo kutumia gari la halmashauri kwa matumizi yake binafsi.

Kulingana na barua inayosambaa kwenye makundi ya whatsapp, kanuni za kudumu za Halmashauri ya Manispaa ya Iringa za mwaka 2015, zinamwagiza mkurugenzi baada ya kupokea maombi ya tuhuma zinazomkabili meya, anatakiwa kupewa taarifa na kuandaa majibu ndani ya siku tano.

“Baada ya kupokea utetezi wako, Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa atamwarifu mkuu wa mkoa tuhuma zinazokukabili pamoja na utetezi wako,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo inafafanua kuwa timu ya uchunguzi baada ya kukamilisha kazi yao na kuisasilisha taarifa hiyo kwa mkuu wa mkoa, kiongozi huyo atairejesha kwa mkurugenzi wa manispaa ndai ya siku 14 kisha itapelekwa kwenye baraza la madiwani kwa ajili ya uamuzi wa tuhuma husika.

“Hivyo nakuomba upokee tuhuma zinazokukabili na unatakiwa kujibu ndani ya siku tano tangu tarehe ya barua hii na majibu ya utetezi yafike ofisi ya mkurugenzi,” inasema sehemu ya Barua.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz