Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alichojibu Zitto tishio la ACT-Wazalendo kufutwa

48771 Alichosemapic

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amefafanua mambo matatu waliyoandikiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Jana Jumatatu Machi 25, 2019 Msajili wa Vyama vya Siasa alikiandikia barua chama hicho na kukipa siku 14 kujieleza kwa nini kisifungiwe kutokana na kufanya mambo matatu.

Mambo hayo ni pamoja na kutumia maneno ya dini ya Kiislam ‘Takbir’ wakati watu wanaodaiwa kuwa ni wanachama wa ACT-Wazalendo walipokuwa wakipandisha bendera ya chama hicho.

Katika barua hiyo iliyosainiwa na naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza ilisema kuwa wanachama wa chama hicho pia walichoma bendera za CUF jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kutowasilisha taarifa ya hesabu za mwaka wa fedha  2013/14 zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Katika mkutano wake na waandishi wa habari leo Jumanne Machi 26, 2019 jijini Dar es Salaam, Zitto amesema madai ya kutowasilisha hesabu za mwaka 2013/14 hayana ukweli wowote.

Amesema wajibu wa chama cha siasa ni kuwasilisha hesabu zake kwa CAG na za mwaka 2013/14 ziliwasilishwa kama walivyotakiwa.

Amefafanua kuwa kilichotokea ni kuwa chama hicho kilipata usajili wa kudumu Mei 5, 2014 ikiwa ni miezi miwili kabla ya mwaka wa fedha kuisha Juni 30, 2014.

Ameeleza kuwa kwa kutumia kanuni za kimataifa za hesabu na ushauri wa CAG, waliambiwa wanaweza kuunganisha hesabu za mwaka wa fedha 2013/14 na 2014/15 kwenye ripoti moja ikiunganisha miezi miwili ya taarifa ya mwaka 2013/14.

"Sheria inaruhusu kufanya hivi hata kwa miezi 18 na kabla ya kufanya hivyo tulimwandikia Msajili wa vyama vya siasa barua ya Januari 22 na 29, 2015 na tukajibiwa, barua zote tunazo," amesema Kabwe.

Amesema chama hicho kilikuwa namba moja kupeleka mahesabu yake kwa CAG kukaguliwa na kupata hati safi.

"Msajili angekuwa na nia njema angeweza kuuliza, labda barua zilipotea ofisini kwake tungempa kwa sababu tunazo na sheria ya vyama vya siasa iliyopitishwa hivi karibuni inampa mamlaka ya kuomba nyaraka zozote, tungempa," amesema Kabwe.

Kuhusu kuchoma bendera za CUF Kabwe amesema kuwa msajili mwenyewe anaonyesha hana uhakika kama kweli waliofanya hivyo ni wanachama wa ACT-Wazalendo.

Amesema chama kina orodha ya wanachama na wanapewa kadi, hivyo wana dhamana na wanachama wao na kwamba msajili alipaswa  ajiridhishe anaowatuhumu ni wanachama wa ACT-Wazalendo.

"Nina uhakika hawezi kwenda mbele ya mahakama kuthibitisha hilo," amesema Kabwe.

Kabwe amefafanua kuhusu matumizi ya neno takbir, kuwa ni jambo lililowashangaza, kwa sababu chama hicho ni chama cha watu wote ikiwamo wenye dini na wasiokuwa na dini.

Amefafanua kuwa kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho imeonyesha wazi kuwa hawafungamani na dini yoyote ndiyo maana wameruhusiwa kufanya shughuli za siasa.

"Tunafahamu Watanzania wana dini zao, maneno yao ya kawaida kutumika hayana maana ya udini, viongozi wote hufungua hotuba zao kwa kusema bwana Yesu asifiwe, tumsifu Yesu Kristo na Assalam aleykum, hatuamini kama kusema hivyo ni udini" amesema Kabwe.

Amesema jambo hilo wanawaachia wanazuoni walifafanue  kama Mwislamu akisema takbir ni udini. "Sheikh Mkuu atoe fatua kuhusu neno hilo." amesema Kabwe.

Kabwe ametoa msimamo wa chama kuhusu barua hiyo kuwa hauna nia njema na wapenda demokrasiaa wote walione kama suala linaloweza kuharibu usalama wa taifa na linaweza kuleta machafuko nchini.

Amesema amani na utulivu  uliopo ni kwa sababu wananchi wana chaguo akichoshwa na CCM atakwena Chadema, CUF na kwingineko.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz