Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alama alizoacha Askofu Kweka KKKT

Askofu Kwekaaaa.png Alama alizoacha Askofu Kweka KKKT

Wed, 29 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Miaka 58 ya utumishi wa Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Erasto Kweka yameacha alama nne zitakazobaki kuwa fundisho katika kukuza huduma ya kanisa hilo.

Dk Kweka (89) alifariki dunia katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Novemba 25 mwaka 2023, alipokuwa akipatiwa matibabu.

Alama hizo zimewekwa wazi leo, Novemba 29, 2023 wakati wa ibada ya kuaga mwili wake katika Kanisa Kuu la KKKT Azania Front, Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), kabla ya mwili wake kusafirishwa kwenda Moshi, mkoani Kilimanjaro yatakapofanyika maziko Desemba 6, mwaka huu.

Katika sehemu ya mahubiri yake, Askofu Alex Malasusa amesema enzi za uhai wake, Dk Kweka alipenda kufanya kazi ili kujipatia kipato chake na hakupenda kuwa ombaomba.

“Baba askofu Kweka alipenda kufanya kazi mwenyewe, tunafikiri kwamba unapokuwa mtumishi wa Mungu unakuwa na haki ya kunyoosha mkono tu (kuomba) lakini kumbe unaweza kuingia mfukoni na kunyosha mkono kwa maskini, Askofu Kweka alikuwa nalo hilo,” amesema Malasusa.

Malasusa ambaye ni Mkuu wa Kanisa hilo Mteule, ameongeza: “Watu wanatafsiri sadaka wanavyoweza ili ziwe faida kwao, lakini haikuwa kwa Baba askofu Kweka. Kuna watu sasa hivi tunaweza kuwalaumu hawaji kanisani labda wanaogopa kuombwa ombwa. Kweka aliondoa dhana ya mtumishi wa Mungu ni maskini. Ningetamani tujifunze dhana ya utumishi huu.” amesema

Alama nyingine alizotaja Askofu Malasusa ni kiwango cha juu cha unyenyekevu licha ya Mungu kumuinua kwa kuwa maarufu ndani na nje ya nchi kutokana na huduma yake.

“Alikuwa mnyenyekevu kuliko jina lake lilivyokuwa, wengine tunatukuka kidogo tu lakini unyenyekevu unakuwa ni F (akimaanisha sifuri), siku moja alinipigia simu akaniambia ‘Baba Askofu samahani kwa kukusumbua sijui naweza kuongea na wewe...sasa mimi na samahani yake wapi na wapi?” ameeleza na kuhoji Askofu huyo.

Alama ya tatu ni kwamba marehemu Dk Kweka alikuwa kiongozi mwenye misimamo na asiyependa mzaha katika kuzingatia umuhimu wa muda pamoja na kuwa na kiwango cha juu cha uaminifu.

“Alikuwa mwaminifu, alikuwa ni miongoni mwa wachache kuujua wokovu, aliwabeba sana wanauamusho ndani ya kanisa,” amekumsha Malasusa.

Katika nafasi hiyo ya uaminifu, Askofu Malasusa amesema kiongozi huyo alitumia muda mwingi kuandika, kuhariri, kusimamia na kuhamasisha washarika kushiriki ibada za kila siku na kwamba hata kabla ya kifo chake, aliomba jeneza lake lisiwe na mbwembwe za mapambo mengi.

“Aliasisi pia uwepo wa masista wa kanisa na huduma za diakonia, Mungu anatamani kuishi kwetu tuache alama, tumtumikie kwa nguvu, mchungaji mwenzetu huyu amemaliza kazi vizuri, je mimi na wewe watu watasema nini?” amehoji huku akiwataka maelfu ya washarika hao kusherehekea utumishi wa Dk Kweka.

Viongozi mbalimbali wa kisiasa na maaskofu wa madhehebu ya kikristo wameshiriki tukio hilo la kuaga mwili huo kwa salamu za rambirambi.

Utumishi wake

Enzi za uhai wake, Dk Kweka alifanikiwa kushika nafasi ya uchungaji mwaka 1965 kabla ya kuwa Msaidizi wa Askofu. Alikuwa Askofu wa pili wa Dayosisi ya Kaskazini, akipokea nafasi hiyo baada ya kifo cha Askofu Dk Stephano Moshi na aliongoza kuanzia mwaka 1977 - 2004, alipokabidhi kiti hicho kwa Askofu Dk Martin Shao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live